Matumaini ya Makubaliano ya Tabia Nchi Lima
1 Desemba 2014Mkutano wa kilele ulioshindwa kuleta tija mjini Copenhagen mwaka 2009 ulifuatiwa na miaka mitano ya hali ya kuvunjika moyo na watu kutojua la kufanya-lakini mwaka huu wa 2014 watu wamepania kuibadilisha hali hiyo. Mada kuhusu hifadhi ya tabia nchi imerejea tena katika ajenda za mazungumzo ya kimataifa. Ingawa utapita muda wa mwaka mmoja hadi mkataba mbadala wa itifaki ya Kyoto utakapotiwa saini mjini Paris, hata hivyo mwaka huu hatua kadhaa muhimu zimefikiwa kuelekea juhudi za kupunguza kiwango cha moshi wa sumu unaochafua mazingira.
Tayari mwezi wa Septemba mwaka huu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon alidhihirisha umuhimu wa mada hiyo. Aliitisha mkutano maalum wa kilele kuhusu tabia nchi mjini New York. Mkutano huo ulifuatiliwa na maandamano tangu nchini Marekani mpaka katika sehemu nyengine za dunia. Kufumba na kufumbua likachipuka vuguvugu la wanaharakati dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Matokeo yake: Marekani na China nchi mbili zinazotoa moshi mwingi wa viwandani zikaelezea utayarifu wao wa kujiunga pia na hatua za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimita 20 tangu miaka 100 iliyopita
Ripoti ya hivi karibuni ya baraza la tabia nchi ulimwenguni haifichi inazungumzia kinaga ubaga umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka" anasema Professor Stefan Rahmstorf wa taasisi ya utafiti wa tabia nchi ya mjini Postdam, Ujerumani. Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita vipimo vya ujoto vimepanda kupita kiasi na kima cha bahari mnamo muda huo huo kimeongezeka kwa sentimita 20. Milima ya barafu katika bahari ya kaskazini ya Arktis imeanza kuyeyuka na kuchangia katika kuongezeka kina cha bahari, na kusababisha majanga makubwa ya kimaumbile."Anasema Prof. Stefan Rahmstorf.
Madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanaonyesha kuzingatiwa na kila upande na hima kutolewa juhudi zizidishwe kuhakikisha moshi wa viwandani haupindukii nyuzi joto mbili za Celsius kwa mwaka.Hilo likishindikana wataalam wanahofia hali ya ujoto inaweza kuongezeka na kufikia nyuzi joto nne za Celsius.
Matumaini ya makubaliano ya tabia nchi kuanza kufanya kazi mwaka 2020
Mkutano wa kilele wa tabia nchi mjini Lima nchini Peru unaangaliwa kama sehemu ya utaratibu mkubwa wa maendeleo anasema mkuu wa baraza la Tabia nchi la Umoja wa mataifa bibi Christiana Figueres. Majadiliano ya kisiasa yameshaanza,wajumbe mjini Lima wanabidi hivi sasa wapige hatua mbele kuelekea makubaliano ya kimataifa ya tabia nchi ili yaweze kutiwa saini mwezi decemba mwaka 2015 mjini Paris na kuanza kufanya kazi mwaka 2020. Hadi Machi mwakani nchi zina wakati wa kuwasilisha ridhaa zao kuhusu hifadhi ya tabia nchi.
Mwandishi:Quaille,Irene/Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Josephat Charo