1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini mapya kwa sarafu ya Euro

22 Julai 2011

Baada ya jana viongozi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro pamoja na sekta binafsi, kufikia makubaliano juu ya Ugiriki ili kuizuia isifilisike, masoko ya hisa yameimarika na Thamani ya sarafu ya Euro kuongezeka.

https://p.dw.com/p/121fi
Rais wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro Jean-Claude JunckerPicha: picture alliance/dpa

Makubaliano hayo yaliyofikiwa jana mjini Brussels, Ubelgiji na viongozi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro ya kuipatia Ugiriki mkopo mpya wa kiasi cha Euro bilioni 159  ili kuizuia isifilisike, na pia kuzuia mgogoro huo wa kifedha usienee zaidi, yamepokewa kwa shangwe katika masoko ya hisa barani Ulaya na Asia, katika biashara zilizofanyika mapema leo asubuhi.

Deutschland Finanzkrise Börse in Frankfurt Börsenkurve
Masoko ya hisaPicha: AP

Hali hiyo inaifanya sarafu ya Euro kuimarika baada ya wiki kadhaa za mgogoro ambao uliifanya pia Italia na Hispania kuingia katika kitisho hicho cha madeni.

Viongozi hao pia walikubali kubeba gharama ya kuyashawishi mabenki yapate hasara katika mpango huo wa kuiokoa Ugiriki na kitisho cha kufilisika, ikiwa ni mwaka mmoja tangu nchi hiyo kupatiwa mkopo wa kwanza ambao haukukidhi mahitaji yake.

George Papandreou Griechenland Krise
Waziri mkuu wa George PapandreouPicha: dapd

Iwapo Ugiriki ingefilisika ingekuwa historia kuwa taifa la kwanza, kufanya hivyo tangu sarafu ya Euro ianzishwe miaka 12 iliyopita.

Kufuatia nchi hiyo kuokoka na kitisho hicho, magazeti ya nchi hiyo pia hii leo yameupongeza mpango huo mpya wa uokozi uliofikiwa jana na kuelezea kuwa kama ni mpango muhimu wa kufa na kupona kwa nchi yao, kutokana na msukosuko wa kiuchumi unaokabili nchi hiyo, lakini pia yameonya kwamba mgogoro huo bado kumalizika kwa sasa.

Naye, Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, amesema kwa maamuzi haya yote wameonesha kwamba hawatayumba katika kulinda muungano waou wa fedha na sarafu ya pamoja.

Kufuatia makubaliano hayo pia wawekezaji nchini Ugiriki wameelezea pia kuongezeka kwa mapato hii leo katika masoko ya fedha.

Naye Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso amesema kwa mara ya kwanza katika mzozo huu misimamo ya kisiasa na ya masoko imekuwa ya pamoja.

Amesema kwa sasa wanatarajia kila mmoja kulinda na kuutekeleza mpango huo.

Akizungumzia mafanikio baada ya makubaliano hayo kufikiwa hapo jana, waziri mkuu wa Italia Silvia Berlusconi ambayo nchi yake pia ilikuwa hatarini kukumbwa na kitisho hicho cha madeni amesema mataifa yote yanayotumia sarafu ya Euro yameweza kuweka tofauti zao pembeni za maslahi ya taifa na kutoa kipaumbele kwa mataifa ya Euro yasiweze kufilisika.

Nchi hizo za mataifa ya Euro pia zimeongeza muda wa kurejesha mkopo na kupunguza kiwango cha riba kwa Ugiriki, Ireland na Ureno.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp. Reuters, dpa)

Mharirii: Miraji Othman