1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wakubaliana kuhusu mkopo mpya kwa Ugiriki

22 Julai 2011

Viongozi wa eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya euro wamekubaliana jana Alhamis kumimina kiasi cha euro bilioni 159 nchini Ugiriki, ikiwa ni mkopo mwingine mpya.

https://p.dw.com/p/121UK
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipowasili kwa ajili ya mkutano huo wa dharura mjini Brussels .Picha: picture alliance/dpa

Viongozi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro walikutana jana hadi usiku mjini Brussels kuzungumzia njia za kuikwamua Ugiriki kutokana na mzigo wake mkubwa wa madeni.

Viongozi wa eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya euro wamekubaliana jana Alhamis, kumimina kiasi cha euro bilioni 159, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa sekta ya binafsi, nchini Ugiriki kuzuwia hali ya kuenea kwa mzozo huo katika umoja wa Ulaya, hata ikiwa kuna kitisho cha kuzusha hali ya kushindwa kulipa madeni. Sekta ya fedha ya binafsi imekubali kutoa kiasi cha euro bilioni 50 ambazo zitaongezwa katika kitita cha euro bilioni 109 kutoka katika serikali za mataifa ya Ulaya pamoja na shirika la fedha la kimataifa IMF, katika makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa dharura mjini Brussels jana.

Tumeonyesha kuwa hatuwezi kuyumba katika kuutetea umoja wetu wa sarafu na sarafu yetu ya pamoja, amesema rais wa umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy.

China EU Präsident Herman Van Rompuy in Schanghai
Rais wa umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy ameukaribisha mpango wa pili wa kuiokoa Ugiriki.Picha: dapd

Kitisho hiki kinapaswa kudhibitiwa, ama sivyo hali ingeweza kutupeleka katika upotevu mkubwa wa imani katika sarafu yetu ya pamoja na huenda hata ingeharibu hali inayoendelea ya ufufuaji wa uchumi katika bara la Ulaya na dunia kwa jumla.

Nafurahi kutangaza kuwa tumepata jibu la pamoja katika mzozo huu. Mkutano wetu ulilenga kwa viongozi wa Ulaya kuulinda uthabiti wa kifedha wa eneo la euro. Leo hii tumefikia maamuzi matatu muhimu, ambayo yanaungwa mkono kikamilifu nasi. Tumeimarisha uwezo wa Ugiriki kuendelea kukopa. Tumechukua hatua kuzuwia hatari ya kuenea kwa mzozo huu. Na mwisho tumeweka nia ya kuimarisha uwezo wa utendaji katika mzozo wa eneo la euro.

Kama sehemu ya mpango huo , eneo la euro litatoa kwa Ugiriki kiwango cha chini cha riba na kurefusha muda wa kuiva kwa dhamana , ili kuweza kuimarisha uwezo wa kubeba deni hilo pamoja na uwezo wa upatikanaji wa fedha nchini humo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mkutano huo.

Sekta ya kifedha imeonyesha kuwapo kwao tayari kuisaidia Ugiriki kwa misingi ya hiari, taarifa hiyo imesema, ikiwa ni kipengee muhimu juu ya vipi makubaliano hayo yanavyoangaliwa na masoko , ambayo yanaweza kufikiria kuwa makubaliano hayo ni njia muhimu kwa Ugiriki kuacha kulipa madeni yake.

Mabenki ya binafsi yametoa mpango wa kubadilishana na kuongeza muda wa malipo kwa madeni ya Ugiriki, ambapo nchi hiyo itaweza kuhifadhi kiasi cha euro bilioni 50 katika muda wa miaka mitatu, taasisi ya kimataifa ya fedha IIF imesema jana.

Belgien EU Griechenland Finanzkrise George Papandreou
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou ameyashukuru mataifa ya Ulaya kwa kuisaidia nchi yake .Picha: dapd

Mabenki hayo pia yametoa wito kwa Ugiriki kuongeza juhudi zake maradufu katika mageuzi ya kiuchumi. Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Manuel Barroso amesema.

Tulihitaji mpango wa kuaminika, tumeupata. Unashughulikia maeneo yote ya wasi wasi wa masoko pamoja na raia. Unashughulikia pia wasi wasi wa mataifa wanachama katika eneo la sarafu ya Euro.

Mkuu wa shrika la fedha la kimataifa IMF Christine Lagarde ameuparibisha mpango wa pili wa kuiokoa kiuchumi Ugiriki na kusema shirika lake litaendelea kufanya wajibu wake. Nae mkuu wa benki kuu ya umoja wa Ulaya Jean-Claude Trichet ameyakaribisha makubaliano ya kuiokoa Ugiriki na kusema kuwa ni hatua muhimu katika kuiimarisha nchi hiyo kifedha.

Mwandishi : Sekione Kitojo.