1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaitikisa Gaza huku msaada wa kiutu ukisubiriwa

20 Oktoba 2023

Israel imeyashambulia kwa makombora maeneo ya kusini mwa Ukanda wa Gaza huku kukiwa na matumaini madogo juu ya kuanza kuingia kwa msaada wa kiutu kwenye ukanda huo uliotarajiwa leo Ijumaa (20.10.2023).

https://p.dw.com/p/4Xn1P
Mzozo wa Gaza na Israel
Moshi ukifuka baada ya shambulizi la Jeshi la Israel kwenye Ukanda wa GazaPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Wapalestina wamearifu juu ya mashambulizi makali ya makombora yaliyofanywa na vikosi vya Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza eneo ambalo waliamriwa kukimbilia kutafuta hifadhi.

Mji wa Khan Younis ndiyo umelengwa tangu mapema asubuhi huku magari ya wagonjwa yakiwabeba wanaume, wanawake na watoto waliojeruhiwa kwenda hospitali ya mji huo ya Nasser ambayo tayari  imezidiwa na wagonjwa na watu wanaotafuta hifadhi.

Jeshi la Israel limesema tangu leo alfajiri limeyalenga zaidi ya maeneo 100 ndani ya Ukanda wa Gaza yanayohusishwa na kundi la wanamgambo wa Hamas. Limesema makombora yalizishambulia ngome za maficho ikiwemo mahandaki na maghala ya kuhifadhi silaha yanayotumiwa na Hamas.

Kiasi watu milioni moja wa Ukanda huo wamepoteza makaazi huku idadi kubwa ikiwa ni ya wale waliotii agizo la Israel la kuondoka kaskazini kwa Gaza. Hospitali nyingi zimeelemewa na kuna mgao wa mahitaji muhimu ikiwemo vifaa tiba na mafuta ya kuendesha majenereta.

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa baadhi ya madaktari kwenye hospatali za Gaza wanafanya upasuaji kwa kutumia mwanga wa tochi za simu na hata kutumia siki kutibu majeraha.

Matumaini ya msaada wa kiutu kuanza kuingia Gaza yanajikokota 

Makubaliano ya kupeleka  msaada muhimu wa kiutu Ukanda wa Gaza yalitarajiwa kuanza kufanya kazi hii leo lakini hadi mchana huu hakuna lori lililovuka mpaka kuingia kwenye eneo hilo.

Wakaazi wa Gaza wakipanga foleni kusubiri mgao wa maji
Wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa mahitaji ikiwemo maji, chakula na nishati Picha: Mohammed Abed/AFP

Umoja wa Mataifa umesema shehena ya kwanza ya msaada huenda itaingia kesho kupitia mpaka wa Rafah ulio kati ya Gaza na Misri.

Mkuu wa Misaada wa Umoja huo Martin Griffiths amewaambia waandishi habari mjini Geneva kuwa wanakamilisha majadiliano ya mwisho na pande zote husika kuhakikisha shughuli za utoaji msaada zinaanza mara moja ndani ya Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye amewasili mchana huu huko rasi ya Sinai iliyo karibu na mpaka wa Rafah katika kile kinachotizamiwa kusukuma miito ya kufunguliwa mpaka huo ili misaada ianze kuingia Gaza.

Kwa upande Misri inayodhaniwa kuwa na jibu la uhakika kuhusu kufunguliwa kwa mpaka wa Rafah imesema matarajio yalikuwa utafunguliwa leo lakini serikali inahitaji muda kukarabati barabara zilizoharibiwa kabla ya kuruhusu malori ya misaada kuanza kuvuka.

Matingatinga yameonekana kwenye ujia wa kukatisha mpaka huu yakifanya kazi ya ukarabati wa barabara.

Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia zataka msaada mkubwa uruhusiwe kuingia Gaza 

Mpaka wa Rafah
Malori ya misaada yakisubiri kwenye mpaka wa Rafah Picha: REUTERS

Kuna zaidi la malori 200 na karibu tani 3,000 za msaada zinasubiri mpakani lakini inatazamiwa ni malori 20 pekee ndiyo yataruhusiwa kuvuka pindi mpaka wa Rafah utakapofunguliwa.

Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia wamesema idadi hiyo ni sawa na "tone la maji" ikilinganishwa na hali ya mahitaji iliyopo Gaza.  

Israel imesema msaada utakaoingizwa ni sharti uwafikie raia peke  na itazuia jaribio lolote la msaada kuangukia mikononi mwa wanamgambo wa Hamas.

Hadi sasa zaidi ya watu 3,785 wameuwawa kwenye Ukanda wa Gaza tangu Israel ilipoanza hujuma zake kujibu shambulizi baya kabisa kuwahi kufanywa ndani ya ardhi yake na wapiganaji wa kundi la Hamas wanaotawala Gaza.

Shambulizi hilo la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya zaidi ya Waisraeli 1,400 na kuwajeruhiwa maelfu wengine. Israel na mataifa kadhaa ya magharibi yameliorodhesha Hamas kuwa la kigaidi.

Kuna matazamio kwamba mzozo huo utazidi makali katika wakati Israel imeonesha ishara zote za kujitayarisha kuingia kijeshi ndani ya Ukanda wa Gaza.

Mzozo huo pia umezusha hasira kwenye mataifa mengi ya Mashariki ya Kati na ulimwengu wa kiarabu.Hii leo Ijumaa kunatazamiwa maandamano kwenye miji kadhaa duniani kupinga hujuma za jeshi la Israel ndani ya Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo serikali mjini Tel Aviv imesisitiza haitoweka chini silaha hadi walitokomeze kabisa Kundi la Hamas.