1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaanga yameingia siku ya 6 nchini Libya

24 Machi 2011

Mashambulizi ya anga yanayofanywa na Majeshi ya Muungano nchini Libya, eo hii yameingia siku ya 6, huku maafisa wa Uingereza wakisema wamefanikiwa kuuvuruga kabisa mfumo wa jeshi la anga la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/10gmJ
Mripuko baada ya mashambulizi ya anga ya vikosi vya Muungano
Mripuko baada ya mashambulizi ya anga ya vikosi vya MuunganoPicha: dapd

Mashambulizi ya hivi karibuni yamefanyika alfajiri ya leo, ambapo milio ya makombora imekuwa ikifyatuliwa kwa mfululizo.

Operesheni hiyo inatekelezwa, wakati ambapo wajumbe kutoka nchi 28 za jumuiya ya Kujihami ya NATO, wakiendelea na mkutano wao nchini Ubelgiji, wenye lengo la kujadili namna jumuiya hiyo itakavyoshiriki katika operesheni hiyo.

Kaimu kamanda wa Kikosi cha Anga cha Uingereza, Greg Bagwell amesema, NATO hivi sasa wamekwisha sikia taarifa za mafanikio ya operesheni inayoendelea.

Afisa huyo ambae ni miongoni mwa waratibu wa operesheni hiyo kwa upande wa Uingereza, amesema kikosi cha anga cha kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi, hakipo katika mfumo wa kivita.

Ndege ya kivita ikijiandaa kushambulia Libya
Ndege ya kivita ikijiandaa kushambulia LibyaPicha: picture-alliance/dpa/Department of National Defence

Marekani imeanza kutabiri kwamba kuendelea kwa shinikizo lililipo sasa kunaweza kumuondoa madarakani Kanali Gaddafi ambaye amekuwa madarakani kwa miongo minne sasa.

Nae Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Libya,kauli aliyoitoa ya kabla ya kufanyika mkutano huo mjini Brussels.

Katika tukio lingine walioshuhudia wamesema wameona miripuko kadhaa usiku wa kuamkia leo katika kambi moja ya jeshi iliyopo karibu na eneo la makazi ya watu ya Tajura umbali wa kilometa 32 mashariki mwa mji mkuu, Tripoli.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari nchini Libya, JANA, mashambulizi hayo ya vikosi vya anga vya muungano yameua idadi kubwa ya watu katika eneo hilo.

Taarifa za shirika hilo limesema ndege za kivita zilifyatua makombora matatu yote yenye athari kwa wakaazi, lakini la mwisho kati ya hayo, lililenga watu waliokuwa wakijaribu kuwaokoa wenzao waliofunikwa na vifusi vya majengo.

Tajura ni ngome muhimu ya kijeshi nchini Libya, na ni eneo la kwanza kushambuliwa na vikosi vya muungano Jumamosi iliyopita, baada ya Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuzuia ndege kuruka katika anga ya nchi hiyo.

Pamoja na tamati ya opereshini ya Libya kutofahamika, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates alipokuwa Misri hivi karibuni alisema kuongezwa kwa shinikizo zaidi dhidi ya Gaddafi kunaweza kuwafanya hata watu wake wa karibu wamgeuke.

Alisema kuna mambo kadhaa ambayo yatajitokeza ingawa siyo rahisi kwa sasa kuyatabiri.

Hata hivyo taarifa kutoka jeshi la Marekani zinasema hivi sasa wapo katika operesheni ya kudhibiti vikosi vya ardhini vya Gaddafi kwa kuwa vimekuwa tishio katika miji inayokaliwa na waasi.

Nguvu mpya ya majeshi ya muungano nazo zimeingia vitani, ambapo usiku wa kuamkia leo ndege ya kivita ya Canada imefanya mashambulizi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Misrata.

Mji huo ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini Libya upo umbali wa kilometa 214 mashariki mwa Tripoli.

Mwandishi: Sudi Mnette/ AFP

Mhariri: Josephat Charo