1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya kuanzisha mashambulizi mashariki mwa nchi hiyo

11 Machi 2011

Mtoto wa kiume wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, Saif al-Islam jana aliapa kuanzisha mashambulizi kamili ya kijeshi dhidi ya vikosi vya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/10XGO
Mtoto wa Kanali Gaddafi, Saif al-Islam al-GaddafiPicha: picture alliance/dpa

Makundi ya waasi wa Libya hayana silaha madhubuti za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na ndege za kivita za Gaddafi, ambazo jana ziliripotiwa kufanya mashambulizi makali katika bandari yenye mafuta ya Ras Lanuf.

Wakati huo huo, mikutano ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya mjini Brussels imeshindwa kuafikiana kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya Libya. Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi, Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen alisema jeshi la muungano litapeleka meli zaidi katika Bahari ya Mediterranean. Pia alisema mipango zaidi inahitajika kabla ya kuanzishwa kwa eneo lenye marufuku ndege kuruka.

Ungarn NATO Außenministertreffen in Gödöllö Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema kuna uwezekano wa Libya kuingiliwa kijeshi, lakini ni mapema mno kuchukua hatua hiyo. Pia Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza kulitambua baraza la upinzani linaloudhibiti mji wa Benghazi, kama mamlaka pekee halali nchini humo, lakini maafisa wa Ujerumani wamesema hatua hiyo ni ya haraka mno.

Pia katika mkutano wao wa jana, Umoja wa Afrika ulikataa wazo la uvamizi wa kijeshi na badala yake umesema utapeleka ujumbe wa wakuu wa mataifa wa umoja huo kujaribu kuandaa makubaliano.