Mashambulizi ya Israel yauwa watu wengine 40 huko Gaza
16 Mei 2021Hayo yanajiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili hali inayotia wasiwasi katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
Mapema Jumapili, Israel ilisema "wimbi la mashambulizi linaloendelea" limeyalenga maeneo 90 kwenye Ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita ikiwemo shambulizi la kombora lililoangusha jengo la ghorofa lililokuwa na ofisi za masharika ya kimataifa ya habari.
Shambulizi hilo limezusha lawama kubwa ya kimataifa.
Kwenye Ukanda wa Gaza idadi ya vifo imeendelea kupanda wakati vikosi vya uokozi viendelea kubaini miili ya watu kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Ndugu wa waliouwawa hawana la kufanya zaidi ya kulia na kuhuzunika.
Guterres aelezea masikitiko yake kwa mapigano yanayoendelea
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "amefadhaishwa" na vifo vya raia huko Gaza pamoja na shambulizi ya Israeli la siku ya Jumamosi lililolilenga jengo lenye ofisi za shirika la habari la Associated Press na kituio cha televisheni cha Al Jazeera.
Jeshi la Israel limesema mapema leo kuwa takribani maroketi 3,000 yamerushwa kutoka Gaza kwenda Israel -- idadi ambayo ni kubwa kuwahi kurikodiwa-- na kati ya hayo 450 yalianguka ndani ya mipaka ya Gaza kutokana na hitilafu za kiufundi.
Bazara la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana jioni ya Jumapili kujadili hali ya mzozo kati ya Israel na Palestina.
Marekani yalaumiwa kwa kushindwa kutuliza hali ya mambo
Marekani ambayo ni mshirika wa Israel na ambayo ilizuia mkutano huo wa Baraza la Usalama kufanyika siku ya Ijumaa, imelaumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua kuzuia umwagikaji wa damu.
Rais Joe Biden wa Marekani alirejea msimamo wake wa kuunga mkono haki ya Israel kujilinda wakati alipozungumza kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Wakati wa mazungumzo hayo Biden alielezea wasiwasi wake kuhusu machafuko yanayoendelea na usalama wa waandishi habari.
Mzozo wa sasa ulichochewa na fujo zilizozuka huko Jerusalem na kusababisha makabiliano makali kati ya polisi wa Israel na Wapalestina wanaopingwa mipango ya kuwahamisha Wapalestina wanaoishi kwenye kitongoji cha Sheikh Jarrah ili kuwapisha walowezi wa kiyahudi.
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Palestina Riyad al-Maliki amezikosoa nchi zilizorejesha au kuanzisha mahusiano na Israel mwaka uliopita ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco.
Kuimarisha uhusiano "bila kufikiwa kwa amani na kukomeshwa kwa ukaliaji wa mabavu wa Israel katika ardhi ya Wapalestina kunamaanisha kuunga mkono utawala wa kibaguzi na kushirika uhalifu wake" amesema Maliki wakati akihutubia mkutano wa dhararu wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu OIC.