Shambulizi la Israel laporomosha jengo la ghorofa 12 Gaza
15 Mei 2021Tukio hilo linatajwa kuwa hatua ya karibuni kabisa ya jeshi la Israel kujaribu kuzima kazi ya kuripoti yanayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza wakati likiendelea kupambana na wanamgambo wa Hamas.
Shambulizi hilo limetokea kiasi saa moja baada ya jeshi la Israel kuamuru watu kulihama jengo hilo ambalo lilikuwa ni ofisi ya shirika la habari la Associated Press, kituo cha televisheni cha Al-Jazeera na ofisi nyingine pamoja na makaazi.
Kombora kutoka ndege za Israel limeliporomosha kabisa jengo hilo la ghorofa 12 na kusababisha wingu zito la vumbi. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu kwanini Israel imelilenga jengo hilo.
Shambulizi jingine kwenye kambi ya wakimbizi
Hayo yamejiri saa chache tangu ndege za Israel zilipofanya hujuma kwenye kambi yenye idadi kubwa ya wakimbizi- kwenye mji wa Gaza na kuwauwa wapalestina 10 wengi wakiwa watoto.
Hilo limetajwa kuwa shambulizi baya kabisa kufanywa na jeshi la Israel katika mzozo unaoendelea sasa.
Kila upande kwenye mapigano hayo unajaribu kutumia nafasi inayopatikana kufanya mashambulizi wakati juhudi za kutaka kusitishwa mapigano zikiendelea.
Mzozo wa hivi sasa ulizuka baada ya kutokea machafuko mjini Jerusalem na kusambaa kwenye kanda nzima huku kukiripotiwa makabiliano kati ya jamii za waarabu na wayahudi kwenye miji mbalimbali ya Israel.
Kulikuwa pia na maandamano ya Wapalestina jana Ijumaa kwenye Ukingo wa Magharibi ambako vikosi vya Israel vilifyetua risasi na kuwauwa watu 11.
Kuna kitisho cha kuzuka vuguvugu jipya la ´Intifada`
Machafuko hayo yanayoongezeka yanatishia kuzuka kwa vuguvugu jipya la Wapalestina ´Intifada´ la kupinga kile kinachotajwa ukatili wa Israel dhidi ya raia wa Palestina.
Leo Jumamosi Wapalestina walikuwa wanaadhimisha kile kinachoitwa nakba kinachomaanisha `siku ya maafa` ambayo hukumbuka karibu watu 700,000 waliofukuzwa kwenye nyumba zake kutoka eneo ambalo sasa ni Israel katika vita vya mwaka 1948 vilivyopelekea kuundwa kwa taifa hilo la kizayuni. Maadhimisho hayo yanaongeza wasiwasi wa kutokea machafuko zaidi.
Mwanadiplomasia wa Marekani Hady Amr aliwasili Mashariki ya Kati siku ya Ijumaa katika juhudi za Marekani za kutafuta suluhu za mzozo unaoendelea.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kesho Jumapili kujadili mapigano ya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo Israel haioneshi dalili ya kuridhia makubaliano ya kusitisha mapigano. Tel Aviv imekataa pekendekzo la Misiri la kusitisha mapigano kwa mwaka mmoja ambalo limeridhiwa na kundi la Hamas linaloongoza Ukanda wa Gaza limeridhia.