1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaharibu barabara ya Lebanon-Syria

4 Oktoba 2024

Lebanon imesema mashambulizi ya Israel ya siku ya Ijumaa (Oktoba 4) yameharibu barabara kuu kuelekea Syria, ambayo Israel inadai inatumiwa na wanamgambo wa Hizbullah kusafirisha silaha kimagendo.

https://p.dw.com/p/4lQ6e
Lebanon | Israel Beirut
Athari za mashambulizi ya Israel nchini Lebabon.Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Mashambulizi hayo ambayo Israel bado haijayazungumzia yamefanyika baada ya watu 310,000 wengi wakiwa raia kutoka Syria kuyakimbia mapigano kati ya Israel na Hezbollah yanayoendelea nchini Lebanon.

Wengi wao wanareja tena Syria kusaka usalama wao, ingawa kwenyewe nako kumekuwa kukishambuliwa mara kwa mara na jeshi la Israel.

Hofu hii imetokana na mashambulizi ya usiku kucha dhidi ya mtaa wenye makaazi ya raia wa Dahiyyah, ambao Israel imekuwa ikidai kuwa ni ngome ya kundi la Hizbullah mjini Beirut. 

Israel inadai Hizbullah inasafirisha kimagendo silaha zake kutoka Syria kupitia mpaka wa Masnaa.

Kulingana na tovuti za Marekani na Israel, mashambulizi hayo pia yalimlenga mrithi wa kundi hilo baada ya kiongozi wake, Hassan Nasrallah, kuuawa wiki iliyopita. 

Soma zaidi: Israel yaendelea kuishambulia Lebanon

Chanzo kimoja kilicho karibu na kundi la Hizbullah kilisema maiti ya Nasrallah imezikwa kwa muda katika eneo la siri hadi pale maziko yake rasmi yatakapofanyika hadharani.

Hatua hiyo imechukuliwa kwa hofu kwamba huenda Israel ingeulenga umati mkubwa wa watu utakaojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyekuwa mashuhuri sana nchini Lebanon. 

Lebanon | Abbas Araghtschi Beirut
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi (kushoto), akipokewa mjini Beirut siku ya Ijumaa (Oktoba 4).Picha: Iranian Foreign Ministry via AP/picture alliance

Israel yajipanga kuishambulia Iran

Mashambulizi haya pia yanafanyika huku Israel ikisema inajadili mbinu za kujibu mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa dhidi yake na Iran wiki moja iliyopita.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliyaita mashambulizi hayo ya Iran kuwa "kosa kubwa", ambalo lingeliigharimu pakubwa Tehran.

Rais Joe Biden wa Marekani alisema siku ya Alkhamis (Oktoba 3) kwamba majibu ya Israel huenda yakajumuisha mashambulizi dhidi ya mitambo ya mafuta ya Iran.

Wakati huo huo, kiongozi wa juu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alitoa hotuba yake ya nandra kwa wananchi wakati wa sala ya Ijumaa akisema mataifa ya Kiislamu yana adui mmoja huku akitetea hatua ya nchi hiyo ya kuishambulia Israel.

"Operesheni nzuri ya vikosi vyetu vya jeshi katika siku mbili tatu zilizopita ilikuwa halali kabisa," alisema Ayatullah Khamenei mbele ya maelfu ya wafuasi wake mjini Tehran.

Iran | Ayatullah Ali Khamenei
Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei.Picha: Iranian Leader Press Office/Anadolu/picture alliance

Soma zaidi: Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel

Waumini waliokuwepo katika Msikiti Mkuu wa Ayatullah Khomeini walionekana wakipeperusha bendera za Mamlaka ya Palestina na za kundi la Hizbullah, huku dua ya kumuombea Nasrallah ikiendelea. 

Katika hotuba yake, Ayatullah Khamenei alisema Marekani na washirika wake wanatumia hoja ya kuilinda wa Israel kama njia ya kuiba rasilimali za Mashariki ya Kati kuelekea mataifa ya Magharibi, lakini alionya kuwa nchi yake haitorudi kwenye upinzani wake dhidi ya utawala wa Israel. 

Mapema wiki hii, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alisema nchi yake haitaki vita na Israel, lakini akaahidi majibu makali zaidi iwapo Israel itafikiria kujibu mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran. 

Haya yanajiri wakati waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran,  Abbas Araghchi, akiwasili mjini Beirut kwa mazungumzo na maafisa wa Lebanon.

Hii ni ziara ya kwanza ya mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kufanyika nchini Lebanon tangu kuuawa kwa Nasrallah. 

afp/ap/reuters