Marekani yatuma timu kuisaidia Nigeria
7 Mei 2014Akizungumza kwa njia ya televisheni, Rais Obama amesema kuwa Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ameukubali msaada wa Marekani kwa lengo la kusaidia kuwakomboa wasichana hao waliotekwa nyara Aprili 14. Rais Obama amethibitisha kuwa Marekani imepeleka timu ya wataalamu wa jeshi, wanasheria na maafisa wa taasisi nyingine kuwatafuta wasichana hao.
Rais huyo wa Marekani amesema nchi yake itafanya kila linalowezekana kuisaidia Nigeria na kwamba malengo ya muda mfupi ya Marekani ni kuisaidia jumuiya ya kimataifa na serikali ya Nigeria, kama timu ya kuhakikisha wasichana hao wanapatikana.
Aidha, amesema katika lengo la muda mrefu, wataangalia namna ya kukabiliana na makundi makubwa kama Boko Haram, yanayosababisha hatari katika maisha ya kila siku ya watu. Amesema jumuia ya kimataifa inapaswa kulitumia tukio hili la kikatili kama msingi wa kuungana na kuliangamiza kundi la Boko Haram.
Wapiganaji wa Boko Haram waliwateka wasichana hao kutoka kwenye shule moja ya sekondari kwenye jimbo la Borno na kuzusha hasira ya kimataifa.
Wasichana wengine watekwa
Taarifa hizo kutoka kwa Rais Obama zimetolewa wakati ambapo wasichana wengine wanane wametekwa nyara na watu wenye silaha jana (06.05.2014) katika kijiji cha Warabe, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Maafisa wa Marekani wana wasiwasi kwamba huenda wasichana hao wenye kati ya umri wa miaka 16 na 18, tayari wameuzwa kimagendo kwenye nchi jirani kama vile Chad na Cameroon. Serikali za nchi hizo mbili zimekanusha madai kwamba wasichana hao wako kwenye ardhi yao.
Akizungumza katika mkanda wa video siku ya Jumatatu, kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, amesema wasichana hao wanashikiliwa kama watumwa kwa ajili ya kuuzwa sokoni.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na haki za binaadamu, imeonya kuwa vitendo vinavyofanywa na kundi la Boko Haram, vinaweza kuhesabiwa kama ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Kundi hilo limesababisha mauaji ya maelfu ya watu nchini humo na limeapa kuanzisha taifa la Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, eneo lenye wakaazi wengi wa Kiislamu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang, amewasili nchini Nigeria kwa ajili ya kuhudhuria Kongamano la Kimataifa kuhusu Uchumi wa Afrika.
Kongamano hilo linafanyika wakati ambapo nchi hiyo inapambana kukabiliana na mashambulizi yanayofanywa na Boko Haram. Kundi hilo linashutumiwa kuhusika na mashambulizi mawili ya mabomu kwenye magari nje kidogo ya mji mkuu, Abuja.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE
Mhariri: Gakuba Daniel