Mamia ya wasichana waliotekwa nyara Nigeria bado hawajulikani waliko
30 Aprili 2014Wazazi waliojawa ghadhabu wameishtumu serikali ya Nigeria kwa kushindwa kuwaokoa wasichana hao waliotekwa nyara kutoka shule moja ya upili katika mji wa Chibok katika jimbo la Borno tarehe 14 mwezi huu.
Shambulizi hilo linaloshukiwa kufanywa na waasi wa Boko Haram ni miongoni mwa mabaya zaidi kuwahi kuripotiwa nchini humo katika kipindi cha hivi karibuni yanayolenga asasi za elimu.
Ghadhabu nchini humo zimeongezeka hata zaidi kutokana na mkanganyiko unaoibuka kutokana na ni wanafunzi wangapi hasa walitekwa nyara na waasi hao na kushindwa kwa jeshi la nchi hiyo kuwapata wasichana hao zaidi ya wiki mbili sasa.
Idadi ya wasichana waliotekwa inatatanisha
Maafisa wa jimbo la Borno wamesema kiasi ya wanafunzi 129 walitekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram waliowalizimisha kuingia katika msafara wa malori na kutorokea msituni na 52 kati ya wasichana hao waliweza kujiokoa
Hata hivyo mkuu wa shule hiyo na wenyeji wa mji huo wa Chibok wanasisitiza kuwa ni wanafunzi 230 waliotekwa nyara na 187 kati yao bado hawajulikani waliko.
Shirika moja liitwalo 'Wanawake kwa ajili ya amani na haki' limewaomba wanawake milioni moja nchini humo kuandamana hii leo katika mji wa Abuja kutaka hatua zaidi kuchukuliwa na serikali katika kuhakikisha wasichana hao wanaokolewa.
Huku maandamano yakipangwa,kuna hofu kuwa wasichana hao walio kati ya umri wa miaka 12 na 17 wamevukishwa hadi nchi jirani za Chad na Cameroon na kulingana na kiongozi mmoja wa Chibok Pogo Bitrus wasichana hao wameuzwa kama wake kwa wapiganaji wa kiislamu kwa thamani ya naira 2,000 ambazo ni sawa na dola 12.
Je wameozwa katika nchi jirani?
Hata hivyo taarifa hizo hazijathibitishwa na serikali ya Nigeria na wizara ya ulinzi imekataa kuzungumzia suala hilo.Baadhi ya wasichana waliofanikiwa kutoroka wameseam walipelekwa katika msitu hatari wa Smabisa ambapo kundi la Boko Haram lina kambi kadhaa.
Boko Haram ambayo jina lake linamaanisha elimu ya maghribi ni haramu imekuwa ikilenga mashule kwa kuyachoma,kuwaua wanafunzi, na kuripua vyuo kwa mabomu.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameshutumiwa vikali kutokana na kuonekana kushindwa kukabiliana na kundi hilo ambalo lilianzisha uasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo miaka mitano iliyopita likitaka eneo hilo kutawaliwa kwa sharia za kiislamu.
Hapo jana wanawake kutoka jimbo la Borno waliokuwa wamevalia mavazi meusi waliandamana nje ya majengo ya bunge wakilia kutaka usaidizi wa kuachiwa huru kwa mabinti zao.
Katika mswada uliowasilishwa hapo jana, bunge la Seneti, limeihimiza serikali na asasi za kiusalama nchini humo kutafuta usaidizi na ushirikiano na nchi nyingine na kutoka kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuimarisha juhudi za kuwaokoa mamia ya wasichana hao.
Mwandishi:Caro Robi/afp
Mhariri: Iddi Ssessanga