1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Marekani yatangaza msaada zaidi wa kifedha kanda ya Sahel

Sylvia Mwehozi
17 Machi 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametangaza msaada wa Dola milioni 150 kwa kanda ya Sahel wakati alipozuru Niger, akitafuta kuimarisha uhusiano na nchi hiyo ambayo imeepuka wimbi la mapinduzi ya kijeshi

https://p.dw.com/p/4OpDl
Niger Niamey | Besuch US-Außenminister Anthony Blinken
Picha: Boureima Hama/AFP

Ziara ya Blinkenimefanyika wakati nchi za Mali na Burkina Faso zikiwa bado katika hali tete na kila moja ikiwa imepitia mapinduzi mara mbili ya kijeshi tangu mwaka 2020. Nchi hizo mbili ambazo ni jirani na Niger, pia zote zimewatimua wanajeshi wa Ufaransa kutoka ardhi yake na kuomba usaidizi wa kijeshi wa Urusi huku kukiwa na ghasia zisizo kwisha zinazofanywa na wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu. Blinken ameitaja Niger kuwa "mfano wa wa ustahimilivu, mfano wa demokrasia na mfano wa ushirikiano" lakini akionya kwamba kuongezeka kwa mamluki wa Urusi katika kanda hiyo hakutakwenda vyema kwa nchi zinazowakumbatia.

Niger Niamey | Besuch US-Außenminister Anthony Blinken
Blinken na waziri wa mambo ya nje wa Niger Hassoumi MassoudouPicha: Boureima Hama/AP/picture alliance

Mara baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Niger Mohamed Bazoum, Blinken alitangaza msaada wa dola milioni 150 kama usaidizi mpya wa kibinadamu kwa kanda ya Sahel ikiwemo Niger moja ya nchi maskini duniani. Ufadhili huo ambao sasa umefikia dola milioni 233 kwa Sahel katika mwaka wa fedha unajumuisha misaada ya chakula na msaada kwa wahamiaji ambao wamekimbilia Libya iliyoharibiwa na vita.

"Msaada huo utasaidia utoaji wa makazi, huduma muhimu za afya, chakula cha dharura, maji salama ya kunywa, usafi wa mazingira, huduma za usafi na pia utasaidia wakimbizi walio hatarini na wanaotafuta hifadhi waliohamishwa Niger. Na lazima niseme, ukarimu wa Niger, wa watu wake kwa wakimbizi wengi, watu wengi waliokimbia makaazi ni wa ajabu. Pia tunaunga mkono uwekezaji katika usalama wa muda mrefu wa Niger", alisema Blinken.

Niger, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imeshuhudia utulivu tangu kurejeshwa kwa demokrasia mwaka 2011 huku tawala za kijeshi zikichukua hatamu katika nchi jirani za Mali na Burkina Faso.Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, afanya ziara nchini Mali

Äthiopien | Permierminister Abiy Ahmed und Anthony Blinken
Blinken alipita Ethiopia na kukutana na waziri mkuu wake Abiy AhmedPicha: Fana Broadcasting Corporate S.C

Mali imeingia kwenye ushirika na Urusi na kuajiri kundi la mamluki la Wagner baada ya wanajeshi wa Ufaransa kuondoka kufuatia operesheni ya kijeshi iliyodumu kwa miaka tisa. Burkina Faso, ambayo ilishuhudia mapinduzi ya mara mbili mwaka jana pekee, pia imetofautiana na Ufaransa, ingawa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo na Urusi wamekanusha madai yakiwemo ya Ghana kwamba kundi la Wagner linaendesha shughuli zake nchini humo.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, watu walio na misimamo mikali ya Kiislamu wamepanua operesheni zao katika kanda yote ya Sahel, eneo lililo chini kidogo ya Jangwa la Sahara barani Afrika. Baadhi ya ghasia mbaya zaidi zimetokea eneo ambalo mipaka ya Niger inakutana na nchi za Mali na Burkina Faso. Niger imeibuka kama mshirika mkuu wa kimataifa katika kanda hiyo wakati ambapo chuki dhidi ya Wafaransa ikiongezeka nchini Mali na Burkina Faso.

Blinken alitembelea Niger baada ya ziara ya siku mbili nchini Ethiopia ambako alisema kuwa taifa hilo linahitaji kupiga hatua zaidi katika utekelezaji wa mkataba wa amani na mkoa wake wa kaskazini wa Tigray kabla ya kurejesha uhusiano wake na Marekani.