Marekani yaikosoa Afrika Kusini kwa kuishtaki Israel ICJ
4 Januari 2024Mathew Miller amesema madai hayo hayapaswi kuchukuliwa kiurahisi na kwamba hadi sasa Marekani, haijashuhudia visa vyovyote vya mauaji ya halaiki katika vita vinavyoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas. Miller amesema bado hana data zozote zinazoonesha ama uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinaadamu umefanyika katika uwanja wa mapambano.
Mapigano yachacha Gaza huku hofu ikizidi juu ya kusambaa kwa vita
Afrika Kusini imewasilisha kesi katika Mahakama ya ICJ iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi, ikiiomba itowe amri ya dharura na kutangaza kwamba Israel inakiuka wajibu wake chini ya makubaliano yaliyowekwa mwaka 1948 kuhusu mauaji ya halaiki.
Kufuatia ombi la Afrika Kusini, sasa mahakama hiyo ya ICJ imepanga kusikiliza kesi hiyo wiki ijayo tarehe 11 na 12.
WHO yalaani shambulio la Israel dhidi ya hospitali Gaza
Hata hivyo, Israel imesema itajitetea dhidi ya madai hayo iliyoyaita yasiyokuwa na "mashiko" huku ikisema Hamas inawatumia raia wa Palestina kama ngao katika vita na kuwapokonya misaada ya kiutu inayopelekwa katika Ukanda wa Gaza, madai ambayo Hamas imeyakanusha vikali.
Marekani yawakosoa mawaziri wa Israel kwa kauli zao nzito
Tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake mjini Gaza Oktoba 7, kujibu mashambulizi ya Hamas yaliyofanywa kusini mwa Israel na kusababisha mauaji ya watu 1,200 wapalestina zaidi ya 22,000 wameuwawa, wakiwemo wanawake na watoto huku wengine takriban milioni 2.3 wakiwa katika mgogoro mkubwa na mbaya wa kibinaadamu mjini Gaza.
Licha ya Marekani taifa kubwa lililo na nguvu duniani kukataa kwamba haijashuhudia visa vyovyote vya mauaji ya halaiki katika mapigano yanayoendelea Gaza, siku ya Jumanne Marekani iliwakosoa mawaziri wawili wa Israel waliotaka Wapalestina wahamishwe kutoka Gaza na eneo hilo kuanzishwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.
Kiongozi wa Hamas asema wako tayari kwa utawala mmoja wa Wapalestina
Marekani ilisema Israel imeihakikishia kwamba kauli za mawaziri hao wawili Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na yule wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben Gvir, haziendani na sera za Israel.
Wakati uo huo, maafisa wengine wa Marekani wamekiri kuwa Wapalestina wengi wameuwawa katika vita hivi huku wakiitolea mwito Israel inayopata msaada wa kijeshi kutoka Marekani kufanya juhudi zaidi kuwalinda raia wakati wa mashambulizi yake dhidi ya kundi la Hamas, ambalo Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Magharibi zimeliorodhesha kama kundi la kigaidi.
afp/reuters