Marekani: Tutarejea katika usuluhishi wa Sudan kwa masharti
1 Juni 2023Tangazo hilo la Marekani limetolewa baada ya jeshi rasmi la Sudan kujiondoa katika mazungumzo na wanamgambo wa RSF, hatua iliyosambaratisha makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano.
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House mjini Washington John Kirby amesema hali mbaya ya usalama inazuia zoezi la kufikisha msaada wa dharura kwa watu wanaouhitaji nchini Sudan, na kukosoa uamuzi wa jeshi kujiondoa katika mazungumzo.
Soma pia: Jeshi rasmi la Sudan lasitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya amani na wanamgambo wa RSF
Duru kutoka Sudan ziliarifu hapo jana, kuwa vikosi vitiifu kwa mkuu wa majeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan vilizishambulia kwa mizinga mizito ngome za wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa mji mkuu, Khartoum.