1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Jeshi la Sudan lasitisha mazungumzo na wanamgambo wa RSF

31 Mei 2023

Jeshi rasmi la serikali ya Sudan limesitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya kusimamisha mapigano kati yake na wanamgambo wa Rapid Support Forces RSF yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia

https://p.dw.com/p/4S0VV
Sudan | Waffenstillstand General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: Sudanese Armed Forces/REUTERS

Akizungumza kwa sharti la kutotambulishwa, afisa wa serikali aliyezungumza na shirika la habari la AFP alisema kuwa jeshi la serikali lilichukuwa uamuzi huo kwasababu kundi la RSF halijawahi kutekeleza hata sharti moja la mkataba huo wa muda mfupi wa kusitisha mapigano ambao ulihitaji kuondoka kwa kikosi hicho katika hospitali na majengo ya makazi na pia ukiukaji wa mara kwa mara wa mkataba huo.

Mapigano yazuka tena Khartoum na Magharibi mwa Darfur

Jumatatu jioni, wapatanishi wa Marekani na Saudi arabia walisema kuwa jeshi la serikali na kikosi cha (RSF) walikuwa wamekubaliana kuongeza kwa siku tano muda wa mkataba wa msaada wa kibinadamu ambao ulikiukwa mara kwa mara katika wiki iliyotangulia. Lakini licha ya ahadi zao, mapigano yalizuka tena Jumanne jioni katika maeneo ya Khartoum na eneo la magharibi mwa Darfur.

Vikosi pinzani vyaahidi kudumisha utetezi

Wakati wa ziara ya kutembelea wanajeshi wake katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum siku ya Jumanne, kiongozi wa jeshi la serikali Abdel Fattah al- Burhan, alisema kuwa jeshi liko tayari kupigana hadi kupata ushindi. Kikosi cha wanamgambo cha RSF kikiongozwa na naibu wa Burhan ambaye sasa ni hasimu wake mkubwa Mohamed Hamdan Daglo, kilisema kuwa kitatekeleza haki yake ya kujilinda na kulishtumu jeshi la serikali kwa kukiuka mkataba.

Sudan | General Mohamed Hamdan Daglo | Hemeti
Mohamed Hamdan Daglo- Mkuu wa kikosi cha (RSF) Picha: Akuot Chol/AFP

RSF yasema imejitolea katika mkataba wa amani

Katika taarifa siku ya Jumanne, RSF ilisema kuwa imejitolea katika mkataba wa kusitisha mapigano licha ya ukiukaji wa mara kwa mara kutoka upande wa jeshi rasmi. Mkataba huo wa kusitisha mapigano unafuatiliwa kwa karibu na Marekani na Saudi Arabia ambazo zinasema umekiukwa na pande zote mbili lakini umeruhusu utoaji msaada kwa takriban watu milioni 2.

Umoja wa mataifa wasema zaidi ya watu milioni moja wapoteza makazi

Umoja wa Mataifa, baadhi ya mashirika ya misaada, balozi na sehemu ya serikali kuu ya Sudan, zimehamisha shughuli zao hadi katika bandari ya Sudan ambayo ni kitovu kikuu cha usafirishaji katika bahari ya Shamu ambayo imeshuhudia msukosuko michache. Kulingana na mradi wa unaochunguza maeneo ya mizozo ya kivita, tangu mapigano kuzuka kati ya makundi hayo pinzani mnamo Aprili 15, zaidi ya watu 1800 wameuawa. Umoja wa Mataifa umesema kuwa zaidi ya watu milioni moja wamepoteza makazi na takriban 350,000 wametoroka nchi hiyo kuelekea ng'ambo ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu 170,000 waliokimbilia Misri.