Marekani kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa
12 Desemba 2008Uamuzi huo utategemea maendeleo yatakayopatikana katika majadiliano ya kutayarisha mkataba mpya wa mazingira unaotazamiwa kutiwa saini Copenhagen Desemba ijayo.
Kwa maoni ya Katibu Mkuu Ban,mizozo ya mabadiliko ya hali ya hewa na uchumi,inatoa nafasi kukabiliana na matatizo yote mawili wakati mmoja.Na kutahitajiwa vichocheo vya kimataifa kusaidia kudhibiti mzozo wa fedha ulioenea kila pembe ya dunia .Sehemu kubwa ya vichocheo hivyo iwe katika miradi ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa,kuzalisha nafasi za ajira katika viwanda vinavyozingatia maslahi ya mazingira na kuhimiza juhudi hizo.Kwa ufupi hatua za kupambana na mzozo wa uchumi ziendeleze malengo ya kuhifadhi mazingira.Wakati huo huo juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa zitasaidia kuendeleza malengo ya kiuchumi na jamii.Na hayo hutegemea maamuzi yatakayopitishwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Safari hii Marekani pia inatazamiwa kutoa mchango wake,kwani mwakani itarejea jukwaani kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kama alivyoeleza Seneta John Kerry aliehudhuria mkutano wa Poznan.Amesema, Marekani itashirikiana na jumuiya ya kimataifa kukabiliana na tatizo hilo, serikali mpya ya rais mteule Barack Obama itakaposhika madaraka mwakani.Marekani imeamua kuongoza katika juhudi hizo si kwa maneno bali kwa kutekeleza sera zitakazoidhinishwa.Kwa mfano,kuweka viwango kwa uzalishaji wa gesi zinazochafua mazingira,kuwa na matumizi bora ya nishati au mutumia nishati mbadala.
Kwa sehemu fulani,juhudi za kutayarisha mkataba mpya wa kimataifa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa,zimekwama kwa sababu ya msimamo wa Rais George W.Bush.Yeye anapinga nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda kuwekewa viwango ikiwa nchi zinazoinukia kiuchumi hazitotia saini makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa gesi zinazoharibu mazingira.Hata Seneta Kerry ameonya kuwa Marekani haitotia saini mkataba ikiwa hakutokuwepo suluhisho la pamoja.Kwani China imeshaipita Marekani katika uchafuzi wa mazingira zikifuatwa na Japan na India.
Makubaliano ya mwisho ya mkataba mpya yanatazamiwa kukamilishwa kabla ya mkutano wa Copenhagen nchini Denmark Desemba mwaka 2009.