Marekani kumtuma mjumbe maalum Ethiopia kutuliza vita
3 Septemba 2022Mike Hammer, mjumbe maalum wa Marekani katika pembe ya Afrika "atawasilisha ujumbe kwa pande husika kwamba zijaribu kusitisha mashambulizi na zishiriki mazungumzo ya amani,” amesema Karine Jean-Pierre.
"Tunalaani hatua ya Eritrea kujiunga tena kwenye machafuko hayo, muendelezo wa mashambulizi ya wapiganaji wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF na vilevile mashambulizi yanayofanywa na serikali ya Ethiopia,” aliwaambia waandishi wa habari.
Mapigano yalianza tena wiki iliyopita katika jimbo hilo la kaskazini baada ya miezi mitano ya utulivu. Hali hiyo imeondoa matumaini ya kupatikana suluhisho la amani dhidi ya mzozo huo ambao umedumu kwa miaka miwili, na suluhisho dhidi ya mgogoro wa kibinadamu ambapo maeneo mengi ya Tigray yanakumbwa na njaa.
Ethiopia, Eritrea waanzisha mashambulizi mapya Tigray
"Hakuna suluhisho la kijeshi kwa machafuko hayo, pande zote sharti zijizuie na tunahimiza pande zote kusitisha vita, ili kuwezesha usafirishaji wa misaada na huduma za msingi kwa wanaohitaji,” amesema Jean-Pierre.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema, Hammer ambaye ni mwanadiplomasia wa muda mrefu na ambaye hushughulikia pia Sudan na Somalia ataanza ziara hiyo kuanzia Jumapili hadi Septemba 15.
Atakutana na maafisa wa Ethiopia na wa Umoja wa Afrika pamoja na wanasiasa wengine nchini humo. Hammer alichukua usukani mwezi Juni na mwezi uliofuata, alizuru Ethiopia katika jitihada za kusaidia kuanzisha mazungumzo ya amani, lakini ambayo hayajaanza hadi sasa kufuatia tofauti kati ya serikali na TPLF.
Guterres azitaka Ethiopia na Tigray kusitisha mapigano mapya
Chama cha TPLF ambacho kilitawala siasa za Ethiopia kwa miaka mingi kimesema nchi jirani Eritrea kwa mara nyingine imetuma vikosi Tigray kufanya mashambulizi ya pamoja na vikosi vya Ethiopia
Eritrea imeshutumiwa kwa ghasia mbaya katika mzozo wa Tigray. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema vikosi vya Eritrea viliwaua mamia ya raia mnamo Novemba 2020 katika mji wa kale wa Axum.
Baada ya miezi kadhaa ya kukanusha tarifa kwamba vikosi vya Eritrea viliingia Ethiopia, mnamo Machi 2021, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alikiri uwepo wa vikosi hivyo na kutangaza viondoke mara moja.
(Chanzo: AFPE)