Guterres azitaka Ethiopia na Tigray kusitisha mapigano mapya
26 Agosti 2022Machafuko hayo yamerudisha nyuma juhudi za kurejesha amani na kukabili mgogoro wa kibinadamu katika jimbo hilo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujaric amesema, kwamba kwenye mazungumzo tofautofauti kwa njia ya simu kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed pamoja na mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPFL Debretsion Gebremichael, Guterres alitoa wito wa kuwekwa masharti yatakayowezesha kuanzishwa kwa mazungumzo thabiti ya kisiasa.
Mnamo Jumatano, maafisa wa Tigray walilituhumu jeshi la serikali ya shirikisho la Ethiopia kwa kile walichokiita kuwa ‘kufanya mashambulizi makubwa' kwa mara ya kwanza katika mwaka mmoja kwenye jimbo la Tigray. Serikali hiyo ilijibu tuhuma hizo ikidai vikosi vya Tigray ndivyo vilianza mashambulizi dhidi yao.
Machafuko hayo yalianza Novemba mwaka 2020, na kuua maelfu ya watu katika taifa hilo ambalo la pili barani Afrika kwa idadi kubwa ya watu. Hata hivyo machafuko hayo yalikuwa yametulia katika miezi ya hivi karibuni mnamo wakati mazungumzo ya amani yanayojikokota yakiendelea.
Mkwamo katika mazungumzo ya amani
Wiki iliyopita, msemaji wa Abiy Ahmed aliwatuhumu maafisa wa Tigray akidai wamekataa kuyakubali mazungumzo ya amani. Na wiki hii jeshi la Ethiopia liliwatahadharisha wananchi dhidi ya kutoa ripoti za hatua za wanajeshi.
Mnamo Jumatano, Umoja wa Mataifa ulisema vikosi vya Tigray viliingia kwa lazima kwenye ghala la shirika la Mpango wa Chakula Duniani lililoko mji mkuu wa jimbo hilo Mekele, na kuchukua malori maalum 12 ya mafuta ambayo magari ya misaada hutumia husafirisha misaada ya kiutu hadi maeneo yenye mahitaji makubwa.
Mkuu wa shirika la kiutu la Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alilaani kitendo hicho siku ya Alhamisi. Kupitia taarifa alisema malori hayo yalibeba lita 570,000 ya Mafuta ambayo yalipaswa kusaidia Umoja wa Mataifa na washirika wake kutoa misaada ya kiutu.
Viwango vya utapiamlo vyaongezeka
Alitahadharisha kuwa bila ya malori hayo, basi watu wataachwa bila misaada ya vyakula, dawa, na vifaa vingine muhimu, mnamo wakati viwango vya utapiamlo na ukosefu wa chakula ukizidi kuongezeka, hivyo athari zitakuwa nyingi na kubwa.
Ethiopia: Wapiganaji wa Tigray walaumiwa kwa ubakaji
Griffiths alitaka vitendo vya kuzuia au kuvuruga mipango ya utoaji misaada ya kiutu kukomeshwa mara moja, na misaada hiyo ilindwe kote nchini Ethiopia. Alikariri wito wa kurejeshwa kwa huduma za msingi katika jimbo la Tigray, ikiwemo za benki na umeme, ambazo huchangia pakubwa katika kuboresha hali ya kibinadamu katika jimbo hilo.
Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni limesema viwango vya utapiamlo vimeongezeka na kwamba 29% ya watoto wana utapiamlo, na watu milioni 2.4 wanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.
(APE)