1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani iko tayari kujibu mashambulizi yaliyofanywa Saudia

16 Septemba 2019

Rais Donald Trump amesema Marekani iko tayari kujibu mashambulizi yaliyofanywa katika miundo mbinu ya mafuta ya Saudi Arabia, mashambulizi ambayo Marekani imeoinyoshea kidole cha lawama Iran.

https://p.dw.com/p/3Peaj
Donald Trump
Picha: Reuters/K. Lamarque

Mashambulizi hayo yamesababisha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa bei ya mafuta duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais huyo wa Marekani kudokeza kuwaMarekani huenda ikajibu kijeshi mashambulizi hayo yaliyofanywa na ndege isiyo na rubani ambayo yamepunguza uzalishaji mafuta wa Saudi Arabia kwa nusu na kuifanya nchi hiyo ya kifalme pamoja na Marekani kusema kuwa huenda wakaamrisha kutumika kwa hifadhi zao za mafuta iwapo kutakuwa na upungufu.

Katika ujumbe alioutoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump ameandika na hapa nanukuu "Usambazaji mafuta wa Saudi Arabia umeshambuliwa. Kuna sababu ya kuamini kwamba tunamjua mhusika, tuko tayari kabisa kulipiza kwa kutegemea na thibitisho lakini tunasubiri Saudi Arabia iseme inayeamini ndiye mhusika wa shambulizi hili," mwisho wa kunukuu.

Iran imeghadhabishwa na hatua ya Marekani ya kuwatupia lawama

Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamedai kuhusika na mashambulizi hayo katika visima viwili vya mafuta vinavyomilikiwa na kampuni kubwa ya mafuta ya Saudi Arabia, Aramco. Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameinyoshea kidole cha lawama Iran akisema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa mashambulizi hayo yalitokea Yemen.

Saudi Arabien Luftbild Ölanlagen
Picha za setlaiti zinaonyesha kushambuliwa kwa miundo mbinu ya mafuta Picha: U.S. government/Digital Globe/AP

Iran imeghadhabishwa na kauli hiyo ya Pompeo na msemaji wa wizara ya mambo ya nje Abbas Mousavi amesema madai hayo yasiyo na mwelekeo hayana maana.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salmanamesema nchi hiyo iko tayari kujibu mashambulizi hayo aliyoyataja kuwa ya kigaidi. Raia wa Saudi Arabia nao wameelezea kusikitishwa kwao na mashambulizi hayo.

"Haya hayakuwa mashambulizi kwa nchi hii ya kifalme, yalikuwa mashambulizi kwa dunia nzima. Kwa majaliwa yake Mungu Aramco itarudia hali yake na hata iwe zaidi ya ilivyokuwa awali," alisema Ahmed Alanzi mkaazi wa Riyadh.

Bei ya pipa moja imepanda mno na kufikia kiwango cha juu zaidi tangu Julai

Huku hayo yakiarifiwa bei ya mafuta imeongezeka leo kufuatia mashambulizi hayo katika sehemu za uzalishaji za Saudi Arabia. Awali bei zilipanda kwa asilimia 20 kabla kushuka tena.

Saudi Arabien | Prinz Mohammed bin Salman
Mwanamfalme Mohammed Bin SalmanPicha: picture-alliance/abaca/Balkis Press

Bei ya pipa moja la mafuta imeongezeka kwa dola 6 na senti 60 hiyo ikiwa ni karibu asilimia kumi na moja na hiyo ndiyo iliyokuwa bei ya juu kabisa tangu katikati ya mwezi Julai.

Licha ya Marekani kuilaumu Iran ikulu ya White House imesema kuwa huenda Rais Trump bado akakutana na Rais wa Iran Hassan Rouhani katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Iran imesema leo kwamba hakutakuwa na mkutano wowote kati ya Rouhani na Trump.