1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bin Salman: Israel ina haki ya kuishi kwa amani

Caro Robi
3 Aprili 2018

Mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia amesema Israel ina haki ya kuishi kwa amani katika ardhi yao, tamko linaloashiria kubadilikwa kwa mtizamo wa ufalme wa Saudi Arabia kuelekea suala la Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/2vOoN
Saudi Arabien Mohammed bin Salman
Picha: Reuters/A. Levy

Katika mahojiano yaliyochapishwa  na gazeti la Marekani la The Atlantic, mrithi wa mfalme Mohammed bin Salman amesema Wayahudi wana haki ya kuwa na taifa katika ardhi ya mababu zao, ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa mahusiano kati ya Saudi Arabia na Israel.

Nchi hizo mbili hazina uhusiano rasmi wa kidiplomasia lakini mahusiano yameboreka katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Saudia yakoleza uhusiano na Israel

Saudi Arabia ambayo ni kitovu cha Uislamu na palipo maeneo matakatifu haiitambui Israel. Imekuwa ikisisitiza kwa miaka mingi kuwa mahusiano ya kawaida kati yao yatarejea iwapo Israel itaondoka kutoka ardhi ya Waarabu iliyochukua kwa nguvu katika vita vya mwaka 1967 vya Mashariki ya Kati, maeneo ambayo Wapalestina wanatumai watalijenga taifa lao katika siku za usoni.

USA Mohammed bin Salman, Kronprinz Saudi-Arabien & Donald Trump in Washington
Mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohamed bin Salman na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/JE. Vucci

Kuongezeka kwa uhasama kati ya Iran na Saudi Arabia kumechochea fununu kuwa maslahi ya pamoja huenda yakaipelekea Saudi Arabia na Israel kushirikiana zaidi dhidi ya Iran ambayo zinaichukulia kitisho chao kikubwa.

Nchi hizo mbili zinaichukulia Iran kama hasimu wao mkubwa huku wakiichukulia Marekani kama mshirika wao mkuu na zote mbili zinaona kuwepo kitisho kutoka kwa makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu.

bin Salman ambaye yuko katika ziara ya wiki tatu nchini Marekani kutafuta kufikia makubaliano kuhusu uwekezaji na kutafuta uungwaji mkono katika kudhibiti ushawishi wa Iran katika kanda ya Mashariki ya kati amesema anaamini kuwa kila mtu, kokote kule ana haki ya kuishi katika taifa lenye amani na anaamini Waisrael na Wapalestina wana haki ya kumiliki ardhi.

Ila ameongeza wanahitaji kuwa na makubaliano ya amani yatakayohakikisha kuwa kuna uthabiti kwa kila mmoja na kuna mahusiano ya kawaida.

Tangu mwaka 2002, Saudi Arabia imekuwa mfadhili mkuu wa mpango wa kutafuta amani katika nchi za Kiarabu ambao unadhamiria kufikiwa kwa suluhisho la kuwepo mataifa mawili huru ili kuumaliza mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

Hatma ya Palestina itakuwa ipi?

Hakuna kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia anayejulikana kutambua kuwa Israel ina haki ya kumiliki ardhi mbali na haja ya kupatikana makubaliano ya kudumu kati ya Israel na Palestina.

Israel Jerusalem Panorama
Mji wa kale wa JerusalemPicha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

bin Salman amemueleza mhariri mkuu wa gazeti hilo la The Atlantic Jeffrey Goldberg kuwa hana pingamizi ya kidini dhidi ya Waisrael kuishi bega kwa bega na Wapalestina ilimradi maeneo matakatifu ya Waislamu mjini Jerusalem yaani Msikiti wa Al Aqsa unalindwa.

Kiongozi huyo wa Saudi Arabia amesema kuna maslahi mengi wanayo kwa pamoja na Israel, na iwapo kuna amani basi kutakuwa na ushirikiano zaidi wa kimaslahi kati ya Israel na nchi za ghuba. Kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, Saudi Arabia iliiruhusu ndege ya kibiashara ya Israel kupita katika anga zake.

Saudi Arabia ililaani hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kuutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel mwaka jana lakini maafisa wa nchi za Kiarabu wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wakati huo, Saudi Arabia ilionekana kuunga mkono mkakati mpana wa Marekani kuhusu kupatikana amani kati ya Israel na Palestina ambao bado ulikuwa unafanyiwa kazi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman