1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni yetu juu ya tumbuizo la muziki,kuhamasisha ulinzi wa mazingira

9 Julai 2007

Wanamuziki mashahuri duniani kote walipanda majukwaani na kutumbuiza kwa lengo la kuwahamasisha watu juu ya ulazima wa kupambana na ongezeko la joto duniani.

https://p.dw.com/p/CHkH

Baada ya kampeni hiyo kamambe ya muziki ambapo wanamuziki mashuhuri walitumbuiza , takriban kila mtu amesema kuwa ameupokea na ameuelewa ujumbe uliowasilishwa na wanamuziki hao.Na kila mtu ameahidi kutoa mchango wake.

Ujumbe huo ni wazi kabisa: hali ya hewa imebadilika na sasa imefikia kiwango cha kutisha. Hali hiyo imesababishwa na ongezeko la joto.

Lakini pamoja na kutoa ahadi hiyo, si jambo rahisi kwa kila mtu kujua kwa uhakika ni mchango gani hasa anaoweza kutoa katika harakati za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa? Labda kwa kupamba mti .

Lakini ukweli ni kwamba baada ya tumbuizo hilo la muziki kumalizika mwishoni mwa wiki baadhi ya watu walirejea kwenye desturi zao za kawaida. Walioenda katika mikahawa walienda na kuagiza kahawa , na baadae kutupa vikombe vya plastiki barabarani.

Ndiyo kusema si watu wote wanaosimama safu moja na mwasisi wa kampeni hiyo ya muziki, bwana Al Gore aliekuwa makamu wa rais wa Marekani.

Hata wakati wanamuziki wakitumbuiza kulikuwa na watu waliobeba mabango yaliyoandikwa maneno ya kushuku msimamo wa bwana Al Gore.Watu hao wametaka janga la mabadiliko ya hali ya hewa litiliwe maanani zaidi.

Hatahivyo maalfu ya watu nchini Marekani wametia saini malengo saba yaliyopendekezwa na bwana Al Gore juu ya kupambana na ongezelo la joto duniani.

Watu hao wamejiwajibisha kuanza kuyazingatia mapendekezo hayo lakini pia wamewataka viongozi wa serikali nao wawajibike.Na hicho hasa ndicho kiini cha juhudi zote:hata ikiwa kila mtu atajaribu peke yake kutoa mchango wake katika kupambanna na mabadiliko ya hewa, kazi kubwa bado itakuwa ni ya serikali. Watunga sera ndiyo wenye uzito mkubwa. Lazima pawepo dhamira ya kisiasa.

Lazima watunga sera watoe vivutio kwa wananchi vya kuwaelekeza katika mwamko wa ulinzi wa mazingira.

Viwanda havina budi vizalishe bidhaa zitakazozingatia shabaha za kulinda mazingira.Wanamuziki wameshatoa mchango wao kwa kuwahamasisha watu duniani kote juu ya ulazima wa kulinda mazingira.

Sasa ni zamu ya bwana Al Gore , yaani mwasisi wa kampeni hiyo ya mazingira kutoa mchango wake. Ameahidi kuendelea na juhudi za kulinda mazingira kwa kupitia kwenye shirika lake,la mfungamano wa kulinda hali ya hewa- Aliince For Climate Protection.

Lakini kila mtu anatambua kwamba fedha zilizopatikana kutokana na juhudi za wanamuziki hazitakuwa dawa ya pekee.

Dawa ni moja tu:watu wote washiriki katika harakati hizo za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa hata kwa kupamba mti mmoja tu pale walipo.

AM.