Mali yaomba msaada wa dharura kuzuia waasi
11 Januari 2013Wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likikutana katika kikao cha dharura mjini New York kujadili mgogoro huo, watu walioshuhudia wamesema zana za kivita na wanajeshi wa kigeni wameanza kuwasili kwa ndege kuimarisha majeshi ya serikali katikati mwa Mali.
Umoja wa Mataifa wataka kupelekwa kikosi haraka
Kufuatia kikao hicho cha dharura, Umoja wa Mataifa uliamrisha kupelekwa haraka kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Umoja wa Afrika kuzuia waasi hao, lakini mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa alisema rais wa muda wa Mali Dioncounda Traore alikuwa ametuma maombi mahususi ya msaada wa kijeshi kutoka kwa Ufaransa, mtawala wa zamani wa taifa hilo.
Taarifa ya kikao hicho ilisomwa na balozi wa ufaransa katika Umoja wa mataifa, Gerard Araud: "Azimio hili linayaomba mataifa yote wanachama, kutoa msaada wa kutatua mgogoro wa Mali, ukiwemo wa kijeshi na kisiasa, na nasisitiza, kutoa msaada kwa mamlaka ya nchi hii kukomesha kitisho cha ugaidi. Tukio hili linaonyesha tena umuhimu wa kupelekwa kwa jeshi la Umoja wa Afrika kaskazini mwa Mali, na tume ya mafunzo ya Umoja wa Ulaya."
Ansar Dine watishia kusonga mbele kusini
Mapema Alhamisi, Abdou Darda kutoka kundi la Ansar Dine, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wapiganaji wa Kiislamu walikuwa wameuteka mji wa Konna, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Mopti, ambapo walioshuhudia walisema wanajeshi wa serikali walikuwa wakirudi nyuma. Darda alisema kwa njia ya simu kuwa wanadhibiti karibu mji wote wa Konna na kuongeza kuwa walikuwa wanapanga kusonga mbele kusini. Mashahidi walisema wanajeshi walikuwa wanarudi nyuma kuelekea Sevare, karibu na Mopti. Ni katika kituo cha kijeshi cha Sevare, umbali wa kilomita 60 kutoka Konna, ambako walioshuhudia waliona ndege za kijeshi zikishusha silaha na wanajeshi wa kigeni.
Afisa wa serikali ya Mali, akithibitisha kuwasili kwa ndege hizo za kijeshi, alisema zilihusisha ndege moja kutoka nchi ya Ulaya, ambayo iliacha wanajeshi na zana katika kambi ya Sevare. Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa mjini New York wamesema rais Traore alimuandikia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na rais Francois Hollande. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, alisema Ufaransa itatoa msimamo wake leo, lakini alielezea hofu ya nchi yake juu ya hali ya usalama inayozidi kuporomoka.
Mashaka juu ya uwezo wa jeshi la Mali
Kuanguka kwa mji wa Konna ni pigo jingine kwa juhudi za kuwazuia waasi hao wa Kiislamu. Mpaka sasa walikuwa wamebakia kaskazini walikochukuwa udhibiti miezi tisa iliyopita, na ambako mataifa ya magharibi yanahofia wanaweza kupafanya mahala salama kwa magaidi. Wanadiplomasia walisema karibu wapiganaji 1,200 wako umbali wa kilomita 20 kutoka mji wa Mopti, ambao ni njia kati ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi na yale yaliyoko chini ya serikali.
Lakini maafisa wa Umoja wa mataifa wameonya kuwa haitawezekana kupeleka wanajeshi kabla ya mwezi Septemba. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice, alisema mashaka yalionyeshwa katika kikao hicho cha dharura, kuhusu uwezo wa jeshi la Mali.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFPE
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.