1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Mali wasonga kusini

8 Januari 2013

Waasi wa kiislamu wanaodhibiti kaskazini ya Mali wanasonga mbele kuelekea kusini katika maeneo yanayokaliwa na wanajeshi wa serikali. Jeshi la serikali limesema liko tayari kujibu ikiwa waasi hao watashambulia.

https://p.dw.com/p/17Fia
Waasi wa Ansar Dine
Waasi wa Ansar DinePicha: Romaric Ollo Hien/AFP/GettyImages

Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la serikali ya Mali, msururu mrefu wa magari aina ya pick-up yaliyojaa waasi wenye silaha nzito, umeonekana katika mkoa wa Mopti, ambako wanajeshi wa serikali wameweka kambi zao tangu mwezi Machi lilipofanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi. Afisa mmoja wa jeshi la Mali ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waasi hao wanasonga mbele na wameonekana katika sehemu mbali mbali.

Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa jeshi liko tayari kujibu iwapo waasi hao watashambulia.

Shinikizo juu ya mazungumzo

Rais wa Mali, Dioncounda Traore
Rais wa Mali, Dioncounda TraorePicha: AFP/Getty Images

Mchambuzi wa masuala ya ukanda wa Sahel Ahmedou Ould Abdallah amesema kuwa huenda waasi hao wanataka kuiwekea shinikizo serikali.

''Hii ni ishara kwamba waasi hao wamekasirishwa mno na mazungumzo, na ninadhani wanataka kuishinikiza serikali. Magari mengi ya waasi hao yameondoka katika mkoa wa Tumbuktu yakielekea kusini. Ikiwa hakutakuwa na usuluhishi, bila shaka Ansar Dine wataendeleza mashambulizi yao''. Amesema Ould Abdallah.

Ansar Dine, moja ya makundi makubwa yaliyotangaza mwezi uliopita kusimamisha uhasama na serikali, wamekataa kusema chochote juu ya iwapo ilikuwa ikiwapeleka wapiganaji wake, au kupanga mashambulizi. Msemaji wa kundi hilo Sanda Ould Boumama amesema hawawezi kusema walipo wapiganaji wao kwa sababu za kimkakati, na kuongeza kuwa serikali ya Mali inawajibika kuhusu matamshi yake kuhusu kusogea kwa wapiganaji.

Waziri wa ulinzi wa Mali Kanali Yamoussa Camara amekiambia kituo cha Televisheni cha Ufaransa, France 24, kwamba waasi walikuwa wakiwaweka wapiganaji wao kwenye msitari unaoitenganisha sehemu ya kaskazini inayoshikiliwa na waasi, na ya kusini ambayo iko chini ya udhibiti wa serikali.

Mwendo wa kujivuta katika usuluhishi

Juhudi za upatanishi za viongozi wa kikanda hazijazaa matunda
Juhudi za upatanishi za viongozi wa kikanda hazijazaa matundaPicha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP/Getty Images

Viongozi wa kikanda na Umoja wa Afrika wamekuwa wakifanya juhudi kuendeleza mazungumzo na makundi ya kiislamu yenye msimamo wa wastani, na waasi wa jamii ya Tuareg wanaotaka kujitenga, na wakati huo huo wakishinikiza matumizi ya kijeshi kuikomboa kaskazini ya Mali.

Mwezi uliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha mpango wa kutumwa kwa vikosi vinavyoongozwa na Umoja wa Afrika kuwatimua wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida kutoka kaskazini mwa Mali, lakini kikosi hicho hakitegemewi kutumwa kabla ya mwezi Septemba.

Kundi la Ansar Dine limesema hakuna majadiliano kuhusu kuwekwa kwa utawala wa sheria ya kiislamu na uhuru wa kaskazini ya Mali kujiamlia mambo yake yenyewe. Kwa upande mwingine lakini, rais wa Mali Dioncounda Traore amesema Mali itabakia kuwa nchi moja, tena yenye utawala usiochanganya mambo ya dini na siasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir