Mali na Ghana historia itajirudia?
8 Februari 2013Na Nigeria itawania kupata taji lake la kwanza katika bara la Afrika tangu mwaka 1994 siku ya Jumapili katika fainali dhidi ya Burkina Faso.
Nafasi ya tatu
Fainali za kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika zinafikia ukingoni mwishoni mwa juma hili, wakati kesho Jumamosi,(09.02.2013) Ghana inakumbana na Mali katika kuwania nafasi ya tatu. Ghana iliishinda Mali kwa mabao 2-0 katika duru ya kwanza ya ubingwa wa mwaka 2012 na Mali ilirejea tena hatimaye na kuiadhibu Ghana kwa kiwango hicho hicho cha mabao katika kuwania nafasi ya pili mwaka jana.
Mubarak Wakaso aliifungia Ghana bao la penalti na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mali katika duru ya kwanza ya mashindano hayo mwaka huu katika uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth na hapo ndio patakuwa na patashika nyingine kesho baina yao, wakati Tai hao wa Mali watawania kulipiza kisasi.
Mpambano kama huu mara nyingi huamuliwa kutokana na timu ambayo haina mzigo mkubwa wa kisaikolojia, na Mali walikuwa katika hali nzuri zaidi walipokutana na Ghana mwaka jana nchini Guinea ya Ikweta.
Mara hii hata hivyo timu zote zimeumia baada ya Mali kubandikwa mabao 4-1 katika nusu fainali dhidi ya Nigeria mjini Durban na Ghana imepoteza mchezo dhidi ya kikosi kilichozusha maajabu cha Burkina Faso katika uwanja wa Nelspruit baada ya sare ya kutatanisha ya bao 1-1.
Mwamuzi afungiwa maisha
Katika kuchukua hatua za haraka kutokana na makosa kadhaa ya mwamuzi, shirikisho la soka katika bara la Afrika, CAF, limemfungia moja kwa moja refa huyo kutoka Tunisia Slim Jdidi.
Nahodha wa Mali na mtu mwenye mikoba yote ya uwezo wa timu hiyo, Seydou Keita, anaamini kuwa Tai hao walishindwa kula nyama dhidi ya Tai wa kijani wa Nigeria kwa sababu wachezaji wake hawakufanya kazi kama timu kama walivyofanya wakati waliowaangusha vijana wa Afrika kusini Bafana Bafana katika robo fainali.
Lakini mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona anaonya dhidi ya kumnyooshea kidole mtu yeyote katika kambi ya timu hiyo wakati wanajaribu kwa mara ya pili kunyakua medali ya shaba.
Ghana imefikia nusu fainali katika fainali nne zilizopita za kombe la Afrika , lakini imefikia fainali mara moja tu, hii ikiwa na maana kuwa wamekuwa washiriki wa mara kwa mara katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya tatu.
Wanigeria sasa waungana
Mtiririko wa Nigeria hadi kufikia katika fainali ya mwaka huu ya kombe la mataifa ya Afrika, umeiunganisha nchi hiyo ambayo mara nyingi imekuwa katika mtengano wakati wa kujionea fahari katika soka na kutokana na taifa hilo kujikuta mara nyingi likikumbwa na habari mbaya tu , kuna sababu hivi sasa ya kusherehekea.
Hii itakuwa fainali ya saba kwa Nigeria , nchi ambayo inasaka taji lao la kwanza katika kipindi cha miaka 19. Burkina Faso imeingia kwa mara ya kwanza katika fainali ya kombe hilo la mataifa ya Afrika , na inawania kulinyakua katika jaribio lake la kwanza hapo kesho Jumapili katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Burkina Faso imeonesha kiwango cha juu cha soka kuliko ilivyokuwa mwaka 1998 ilipofikia hatua ya nusu fainali nchini mwao. Walionesha pia hali ya kutochoka haraka hata pale walipolazimika kucheza muda wa nyongeza kabla ya kuishinda Togo kwa bao 1-0 katika mchezo wa robo fainali.
Kocha wa kikosi cha Tai wa Kijani, Nigeria , Stephen Keshi sasa atakuwa na fursa kuwa mtu wa pili katika historia ya miaka 56 ya mashindano haya kutwaa taji hili kama kocha na pia mchezaji , akifuata nyayo za Mahmoud El Gohary wa Misri aliyeshinda taji hili mwaka 1959 kama mchezaji, na mwaka 1998 akiwa kama kocha wa Mafarao hao nchini Burkina Faso.
Kocha Stephen Keshi hivi sasa anaonekana kuchukua nafasi ya juu katika soka la Afrika kwa sasa na mashabiki wa Nigeria wanaamini kikosi hicho kilichochanganya damu changa kitafanya maajabu.
Kocha wa Tunisia ajiuzulu
Na shirikisho la kandanda nchini Tunisia limekubali kujiuzulu wadhifa wake kocha Sami Trabelsi wa nchi hiyo kutokana na kushindwa kwa timu hiyo kuvuka kiwango cha michuano ya makundi.
Makocha watatu wamekwisha tajwa kuwania nafasi hiyo. makocha hao ni Nabil Maaloul , ambaye ameiongoza Esperance ya Tunisia kuchukua ubingwa wa Champions League katika bara la Afrika mwaka 2011, Khaled Ben Yahia na Maher Kenzari.
Kocha wa mabingwa wa zamani wa Afrika , Chipolo polo ya Zambia Herve Renard amepigwa faini ya dola 10,000 ambayo hatatakiwa kuilipa mara moja , kutokana na kudai kuwa shirikisho la soka la Afrika limefurahishwa na kuondolewa na mapema mabingwa hao wa zamani kwasababu hawapendezi machoni.
Shirikisho hilo la kandanda la Afrika limesema kuwa limepokea barua ya kuomba samahani kutoka kwa Renard na shirikisho la soka la Zambia lakini bado lilitoa adhabu hiyo ambayo imeahirishwa na pia onyo kali kwa matamshi hayo aliyoyatoa baada ya Zambia kucheza na Burkina Faso Januari 29.
CAF imesema faini hiyo itaondolewa iwapo hakutakuwa na matukio mengine kama hayo kwa muda wa mwaka mmoja.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: