Ndoto ya Cote D'Ivoire yaota mbawa
4 Februari 2013Burkina Faso na Nigeria zimekamilisha orodha ya timu nne zilizosalia katika kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika , AFCON 2013 nchini Afrika kusini jana(03.02.2013) wakati Cote D'Ivoire ambayo ilikuwa inapigiwa upatu kutoroka na taji la mwaka huu la kombe la Afrika ikishindwa kutimiza matarajio hayo.
Burkina Faso iliishinda Togo kwa bao 1-0 baada ya mchezo kuingia katika dakika za nyongeza na Jonathan Pitroipa aliipatia ushindi timu yake katika uwanja wa Nelspruit ambapo kabla ya hapo Nigeria ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tembo wa Cote D'Ivoire katika uwanja wa Rustenburg na kuweka mashindano haya wazi kwa yoyote kwa hivi sasa.
Nusu fainali
Nigeria sasa itapambana na Mali katika nusu fainali mjini Durban siku ya Jumatano na Ghana itakwaana na Burkina Faso uwanjani Nelspruit siku hiyo hiyo, michezo itakayoamua ni timu gani mbili zitaingia katika fainali ya mwaka huu kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika.
Nigeria walipewa nafasi ya asilimia 20 tu ya ushindi na kocha wao Stephen Keshi katika uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace. Lakini bao la Sunday Mba , dakika 12 kabla mpira kumalizika liliendeleza mfululizo wa ndoto za jinamizi kwa Didier Drogba na kikosi kizima cha Tembo wa Cote D'Ivoire ambao walipigiwa upatu kushinda ubingwa wa Afrika mara tano lakini mara zote wamekaribia tu kufanya hivyo.
Ni sababu gani inasosababisha ndoto ya Drogba na kikosi cha Cote D'Ivoire mara nyingi kuota mbawa? Swali hili nilimuuliza Mtemi Ramadhani mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na pia afisa wa zamani wa shirikisho la kandanda la Tanzania TFF, ambaye amerejea hivi karibuni mjini Dar Es Salaam kutoka Afrika kusini ambako alikuwa akihudhuria michezo hii ya kombe la mataifa ya Afrika. Sikiliza mahojiano na Mtemi Ramadhani hapo chini.
Kusikiliza mahojiano na Mtemi Ramadhani bonyeza alama za spika hapo chini:
Didier Drogba na kizazi kinachoitwa cha dhahabu cha wachezaji wa Cote D'Ivoire walitoka uwanjani jana wakiwa vichwa chini baada ya kushindwa kwa mara nyingine tena kutimiza matarajio ya wengi kuwa wanaweza kuvishwa taji la wafalme wa soka katika bara la Afrika msimu huu.
Ndoto yaota mbawa
Kwa Drogba , ambaye anatimiza umri wa miaka 35 mwezi ujao, hii ilikuwa fursa yake ya mwisho ya kulinyakua taji hili la mataifa ya Afrika.
Wachezaji wengine katika kikosi hicho kilichopewa nafasi kubwa lakini kimeshindwa kupata mataji kama Kolo Toure mwenye umri wa miaka 31, Didier Zokora mwenye umri wa miaka 32 na mlinda mlango Boubacar Barry mwenye umri wa miaka 33 , pia nao watakuwa na hisia kama Drogba za kujihisi hawana chao.
Jopo la wataalamu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA litaangalia uwezekano wa kubadilisha namna sheria ya kuotea mpirani ,"offside", inavyotafsiriwa wakati wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo mwezi ujao. Pia FIFA inasema kuwa jopo lake hilo pia litaangalia njia ya kuziba mwanya kuhusiana na mpira wa kuanzishwa na refa kwa kudondoshwa baada ya mpira kusimama kwa muda uwanjani, baada ya Shakhtar Donetsk kufunga goli la kutatanisha dhidi ya Nordsjaelland katika Champions League msimu huu.
Matapeli wa kupanga matokeo
Wakati huo huo polisi katika bara la Ulaya wameonya leo kuwa hadhi ya mchezo wa mpira wa miguu iko katika wakati mgumu baada ya kufichua kuwa wamevunja mtandao wa kihalifu wa kupanga matokeo ya michezo kadha , ikiwa ni pamoja na Champions League na michezo ya kombe la dunia.
Polisi ya Ulaya Europol imesema kuwa uchunguzi uliofanywa katika nchi tano umegundua shaka katika michezo 380 iliyoathirika kutokana na kampuni la kuweka dau na kuagulia nani mshindi, ambalo shughuli zake ambazo ni kinyume na sheria zimesambaa hadi kwa wachezaji, waamuzi na maafisa duniani kote katika viwango vyote vya mchezo huo.
Ligi za Ulaya :
Bundesliga ilikamilisha mchezo wake wa 20 jana Jumapili, ambapo mabingwa watetezi Borussia Dortmund iliponyakua nafasi ya pili katika msimamo wa ligi , baada ya mpambano mkali wa vuta nikuvute dhidi ya Bayer Leverkusen. Borussia Dortmund ilipata ushindi wa mabao 3-2. Kocha wa mabingwa hao watetezi Borussia Dortmund , Jürgen Klopp amesema kuwa huo ulikuwa mchezo mgumu sana kwa mabingwa hao.
Bayern Munich inayoongoza ligi hiyo, ina points 51 kibindoni , ilipata ushindi wa uhakika wa mabao 3-0 dhidi ya Mainz 05 siku ya Jumamosi.
Borussia Dortmund inashikilia nafasi ya pili sasa ikiwa na points 39. Bayer Leverkusen imeteremka hadi nafasi ya tatu ambapo ina points 37.
Premier League
Manchester United iliongeza mwanya wa points kileleni mwa msimamo wa ligi ya Uingereza Premier League hadi points tisa baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fulham na Manchester City ikatoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Liverpool jana Jumapili.
City watamshukuru zaidi mshambuliaji wao Sergio Kun Aguero baada ya kufunga bao zuri ajabu kwa kuuzungusha mpira akiwa katika kibendera cha kona hadi wavuni, na kuipatia timu yake sare muhimu katika wakati ambao City ilionekana kudoda.
Goli alilojifunga mwenyewe Cristiano Ronaldo lilitosha kuwaadhibu mabingwa watetezi wa ligi ya Uhispania La Liga, Real Madrid na kupata kipigo kingine cha bao 1-0 dhidi ya Granada, na kuongeza athari zaidi katika kampeni yao ya kutetea ubingwa wao. Lionel Messi alipachika bao la 12 katika michezo 12 aliyocheza na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Valencia.
Super Mario
Mario Balotelli alipachika mabao mara mbili katika ushindi wa AC Milan mwanzoni mwa mshambuliaji huyo kuichezea timu aliyoishabikia tangu utotoni mwake na kuipa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Udinese. Milan imesogea hadi katika nafasi ya nne ikiwa na pints 40 ikitanguliwa na majirani zao wa Inter kwa tofauti ya magoli. Viongozi wa ligi hiyo Juventus Turin inaongoza kwa points tatu mbele ya SSC Napoli wakati timu zote hizo zilipata ushindi dhidi ya Chievo Verona na Catania.
Tennis:
Uhispania ambayo iko katika nafasi ya juu katika mchezo wa tennis duniani imeondolewa katika duru ya kwanza ya mashindano ya kombe la Davis kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 wakati Milos Raonic alipomshinda Guillermo Garcia-Lopez na kuipa Canada ushindi wa michezo 3-1 katika kundi lao jana Jumapili. Uhispania ambayo ni mabingwa wa kombe hilo mara tano ,ilionekana kupata taabu tangu mwanzo wa pambano hilo mjini Vancouver Canada na Raonic alizika ndoto zao kwa kumshinda Garcia Lopez kwa seti tatu kwa sifuri , 6-3 6-4 na 6-2.
Kwa taarifa hizo mpenzi msikilizaji ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kwa leo. Jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe /
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman