Majeshi yamiminika Mali
17 Januari 2013Azimio hilo linafikiwa wakati huu ambapo Umoja wa Ulaya uko mbioni kuupitisha mpango wa kupeleka wakufunzi wa kijeshi kuvinoa vikosi vya Mali.
Mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa ECOWAS, Aboudou Toure Cheaka, amesema kuwa Nigeria iko tayari kupeleka vikosi vyake nchini Mali ili kusaidia mapambano dhidi ya waasi.
Vikosi hivyo vinatarajiwa kutua nchini Mali katika kipindi cha takriban wiki moja baada ya vikosi vya Ufaransa kuanza operesheni ya kuiokoa Mali kutoka mikononi mwa makundi ya waislamu wenye itikadi kali.
Bwana Cheaka amesema pia kuwa vikosi vingine kutoka Algeria vitapelekwa hii leo katika eneo la mpaka baina ya nchi hiyo na Mali. Pamoja na hivyo, Togo na Burkina Faso nazo zitapeleka wanajeshi wake nchini Mali mwishoni mwa juma hili au mwanzoni mwa juma lijalo.
Vikosi hivyo vinatumwa kuongeza nguvu ya vile vya Ufaransa vinavyowajumuisha wanajeshi 800 ambavyo tayari viko Mali vikipambana na makundi ya waasi. Ufaransa imeahidi kuongeza wanajeshi wake nchini humo na kufikia 2,500 pamoja na vifaa kama vile helikopta za kijeshi, ndege za kivita, ndege za kijeshi za kufanyia uchunguzi kubaini walipo waasi pamoja na vifaru.
Umoja wa Ulaya kusaidia mafunzo ya kijeshi
Mapambano ya kuwatoa waasi nchini Mali yanazidi kupata uungaji mkono wa kimataifa ambapo hii leo mjini Brussels Ubelgiji, Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana kuupitisha mpango wa kupelekwa wakufunzi wa kijeshi kwa ajili ya kuvinoa vikosi vya Mali. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Mali, Tieman Coulibaly, naye anashiriki kikao cha leo mjini Brussels.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye nchi yake inashiriki pia katika kikao cha Brussels alisema kuwa kuna haja ya kuisaidia Mali katika mzozo ilionao.
"Naamini kuwa tuko katika shinikizo la wakati. Ujerumani inaona kuwa usalama wa eneo la magharibi ya Afrika ni sawa na Usalama wake. Bila shaka ugaidi uliopo kaskazini mwa Mali si kitisho kwa Afrika tu bali pia kwa Ulaya" alisema Merkel.
Afisa wa ngazi za juu katika umoja huo amesema kuwa suala la kupeleka wakufunzi hao sasa limekuwa ni la lazima na linatakiwa litimizwe haraka iwezekanavyo na kwamba wanaangalia pia uwezekano wa kupeleka misaada mingine inayohitajika.
Hata hivyo taarifa kutoka umoja huo zinasema kuwa wakufunzi hao hawataanza kazi mara moja hadi hapo hali itakaporejea katika utulivu kwenye eneo la kusini mwa Mali ambapo ndipo vitakapoweka kambi. Vikosi kamili vya mafunzo vinatarajiwa kuingia Mali mwezi Februari mwaka huu.
Umoja wa Ulaya pia unatarajia kuishinikiza serikali ya mpito ya Mali kuufanyia kazi mpango wa kuwa na serikali kamili ili iweze kupata fedha za msaada.
Kwa upande wake Marekani imesema kuwa inaangalia ni aina gani ya msaada iipe Ufaransa ambayo inapambana na waasi nchini Mali. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, amesema kuwa nchi yake haina mpango wa kupeleka vikosi Mali.
Mwandishi: Stumai George/Dpa/Ape/Reuters
Mhariri: Josephat Charo