1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ufaransa waanza mapigano ya nchi kavu Mali

16 Januari 2013

Ufaransa imedhamiria kuwavunja nguvu wanamgambo wa kiislam kaskazini ya Mali.Mapigano ya nchi kavu yanaripotiwa huku juhudi zikiendelezwa kuhusu namna ya kusaidia opereshini za Ufaransa nchini humo.

https://p.dw.com/p/17L7A
Vifaru vya jeshi la Ufaransa vinaondoka Bamako kuelekea kaskazini ya MaliPicha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Mlolongo wa magari ya kijeshi ya Ufaransa yameondoka Niono, umbali wa kilomita 350 kaskazini ya Bamako na kuelekea Diabali ambako kwa ushirikiano pamoja na vikosi vya serikali ya Mali, wanajeshi wa Ufaransa wanawazingira wapiganaji wa itikadi kali katika mji mdogo wa karibu na mpaka wa Mauritania.

Mkaazi mmoja wa Niono amesema amewaona wanajeshi wa Ufaransa na Mali wakiwa ndani ya magari ya kijeshi, wakielekea katika eneo linalodhibitiwa na waasi.

Mkuu wa vikosi vya wanajeshi wa Ufaransa, Edouard Guillaud, akizungumza na kituo cha Radio cha Europe I amethibitisha kuhusu kuanza mapigano ya nchi kavu wakati wowote kutoka sasa.

Mashahidi mjini Bamako wanasema wanajeshi zaidi wa Ufaransa wamewasili leo pamoja na vifaa vyao vya kivita. Zaidi ya wanajeshi 800 wa Ufaransa wanakutikana nchini Mali hivi sasa na idadi yao inatarajiwa kuongezeka na kufikia wanajeshi 2,500.

Ujerumani yaahidi kusaidia

Bundeskanzlerin Angela Merkel Alassane Ouattara Elfenbeinküste
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais Alassane Ouattara wa Côte d'IvoirePicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, madege ya kivita ya Ufaransa yanaendelea kuvihujumu vituo vya waasi kaskazini ya Mali.

Ufaransa imeitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono mapambano dhidi ya wanamgambo wa kiislamu. Rais Francois Hollande amesema ingekuwa Ufaransa haijaingilia kati, basi waasi wa kiislamu wangeweza kuiteka kikamilifu Mali.

Mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya yameahidi kusaidia kwa njia moja au nyengine. Ujerumani imesema inazingatia uwezekano wa kutuma madage kadhaa ya kijeshi kwa ajili ya kuwasafirisha wanajeshi 3,300 wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi, ECOWAS. Kansela Angela Merkel alikutana mjini Berlin na rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya ECOWAS.Katika mkutano na waandishi habari,kansela Angela Merkel amesema kitisho cha ugaidi nchini Mali kinatishia pia usalama barani Ulaya. Baadaye rais Ouattara alizungumza na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle,aliyeahidi msaada wa kiutu wa Euro milioni moja kwa wakimbizi wa Mali waaliokimbilia katika nchi jirani.

Vikosi vya ECOWAS vyatarajiwa kesho Mali

Mali Militäreinsatz 15. Januar 2013
Maafisa wa kijeshi wa nchi za Afrika MagharibiPicha: Reuters

Kwa upande mwingine, wakuu wa vikosi vya wanajeshi wa nchi za ECOWAS wanaendelea na mkutano mjini Bamako kukamilisha mkakati wa kuingilia kati nchini Mali kama ilivyotajwa katika azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa. Nigeria inasemekana inachangia wanajeshi 900, huku mataifa mengine ya ECOWAS yakichangia kuanzia wanajeshi 100 hadi 500.

Mzozo wa Mali unazusha hofu ya kuenea itikadi kali katika nchi za kiislamu za Afrika Magharibi. Rais Macky Sall wa Senegal amewataka raia wake wawe macho. Wakati huo huo, kituo cha mafuta cha Algeria, In Amenas, katika jangwa la Sahara, kimeshambuliwa hii leo. Mtu mmoja ameuwawa na wengine saba kujeruhiwa. Waasi wa itikadi kali kutoka Mali wamedai kuhusika na shambulio hilo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo