Maelfu waandamana Ufaransa kuwaunga mkono Wapalestina
23 Mei 2021Maelfu ya watu waliandamana Jumamosi mjini Paris na katika miji mingine ya Ufaransa kuwaunga mkono Wapalestina kufuatia mgogoro huo wa Mashariki ya kati.
Chama cha wafanyakazi CGT kimesema takriban watu 4,000 walishiriki maandamano hayo mjini Paris.
Maandamano mengine yalifanyika katika miji ya Lyon, Strasbourg, Toulouse na Montpellier kusini mwa nchi hiyo.
Angela Merkel aonya dhidi ya chuki
Nchini Ujerumani maandamano ya kuwatetea Wapalestina yalifanyika katika miji mbalimbali.
Polisi imesema usiku wa kuamkia leo kwamba maandamano hayo iliyoshuhudiwa katika miji ya Berlin, Frankfurt, Giessen na Leipzig, na yalifanyika kwa amani.
Awali Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alionya dhidi ya matamshi ya chuki au matendo ya ubaguzi wa rangi kwenye maandamano hayo kwamba kuchochea chuki dhidi ya Wayahudi na kwa misingi ya ubaguzi wa rangi ni kinyume cha sheria, na matendo kama hayo ni lazima yaadhibiwe vikali.
Mnamo Jumamosi, maafisa wa polisi wa Ujerumani waliwakamata watu 60 wakati wa maandamano hayo mjini Berlin. Maafisa 100 wa polisi walijeruhiwa wakati maandamano yaligeuka kuwa ya vurugu.
Maafisa wa Ujerumani wana wasiwasi kuhusu kuibuka tena kwa matamshi ya chuki kutoka kwa watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia, hasa kufuatia kisa cha Oktoba 2019 ambapo kulikuwa na jaribio la shambulizi katika sinagogi ya Kiyahudi katika mji wa Halle.
Ofisi za serikali Gaza kufunguliwa
Maafisa wa serikali katika Ukanda wa Gaza wanajiandaa kufungua ofisi zao na kuanza kazi tena leo mnamo wakati makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Palestina Hamas yakiendelea kudumishwa. Msemaji wa serikali ya mitaa amesema hayo.
Shughuli za serikali ya mitaa zilisitishwa wakati mashambulizi ya angani ya Israel yalipoanza dhidi ya ukanda huo Mei 10, kujibu makombora yaliyofyatuliwa na wanamgambo wa Hamas kuelekea Israel.
Mashambulizi yaliyoyalenga muundo mbinu wa kijeshi wa wanamgambo wa Hamas pia yaliharibu makaazi ya raia, vituo vya afya na ofisi nyingine za umma, hivyo kuathiri na kukwamisha kabisa maisha ya kila siku katika ukanda huo ulio na zaidi ya wakaazi milioni mbili.
UN: Wakaazi Gaza wahitaji msaada wa dharura
Zaidi ya watu 240 waliuawa Gaza kufuatia mashambulizi hayo ya siku 11, miongoni mwao watoto 66 na vilevile watu 12 waliuawa ndani ya Israel.
Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza, watu wengine 1,910 walijeruhiwa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limehimiza msaada wa dharura kutolewa kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza.
Wanachama wa Baraza hilo wamesisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho la kudumu itakayojikita katika kuundwa kwa mataifa mawili Israel na Palestina.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu wapatao 800,000 katika eneo la Gaza hawana maji safi na takriban asilimia 50 ya mifumo ya maji iimeharibiwa.