1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
6 Agosti 2018

Mjadala kuhusu umuhimu wa kuanzishwa upya mpango wa kutumika jeshini, hali nchini Venezuela na mabadiliko ya tabianchi na athari zake ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari magazetini

https://p.dw.com/p/32fuN
Deutschland Hitze Wetter
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

 

Tunaanzia hapa hapa Ujerumani ambako mjadala umepamba moto ndani ya chama cha Christian Democratic Union-CDU cha Kansela Merkel kudai zoezi la vijana kutumikia jeshi lililositishwa mwaka 2011, lianzishe upya. Maoni yanatofautiana kuhusu suala hilo. Gazeti la "Pforzheimer Zeitung" linaandika: "Ni matarajio ya kila mmoja wetu kuona watu wanapigania kuishi pamoja.Tatizo ni kwamba fursa ya kulifikia lengo hilo imetoweka tangu mwaka 2010/2011. Wakati ule uliibuka mwanya wa kulijadili suala hilo, kwa sababu mpango jumla wa kuwajibika ndilo lililokuwa jibu mbadala kwa zoezi la kutumikia jeshini. Watu waliipoteza fursa ya kuanzisha mjadala wa kina, au tuseme waliikwepa kabisa. Kufutilia mbali wajibu wa kutumikia jeshini na kuanzishwa mpango wa watu kujiunga kwa khiari jeshini ulikuwa uamuzi uliopitishwa kwa pupa bila ya kufikiriwa kwa undani."

Njama ya kutaka kumuuwa Maduro au mbinu ya kung'ang'ania madaraka?

 Nchini Venezuela miripuko miwili ilitokea wakati rais Nicola Maduro alipokuwa akihutubia sherehe za kijeshi mjini Caracas. Maduro anazungumzia kuhusu njama ya kutaka kumuuwa lakini waandishi habari  tangu wa ndani mpaka wa kimataifa wanashuku. Gazeti la "Straubinger Tagblatt/Landshuter" linaandika: "Ni shida kuamini kwamba Nicolas Maduro aliyeitumbukiza nchi yake katika janga la misuko suko, amechaguliwa tena kuwa rais mwezi Mei uliopita. Rais huyo anaezusha mabishano amepoteza tahayuri zote katika kinyang'anyiro cha kung'ang'ania madaraka-miaka kadhaa iliyopita ameandaa njama dhidi ya bunge. Hivi sasa  Maduro analigeuza  tangi la gesi lililoripuka, kama wazima moto wasemavyo, kuwa ni njama ya kutaka kumuuwa."

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi

Joto kali kupita kiasi linapiga katika takriban nchi zote za Ulaya wakati huu wa msimu wa kiangazi. Ndani hakukaliki na nje hakutokeki wanasema wenyewe. Mhariri wa gazeti la kaskazini mwa Ujerumani la "Hannoversche Allgemeine" analeta uwiano kati ya msimu wa kiangazi 2018 na mabadiliko ya tabianchi na kuandika: "Mchanganyiko tunaoushuhudia hivi sasa wa ukame na joto kali ni tukio la sadfa au ni madhara ya mabadiliko ya tabianchi? Mjadala huu haukuanza leo hali kama hii iliyokithiri inapotokea. Umezidi kupata nguvu tangu pale wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia walipoanza kuwatusi wanaharakati wanaopigania usafi wa mazingira . Mjadala unaweza kufupishwa pindi tukizingatia kwa makini hali ya mambo: Mabadiliko ya tabianchi au la, maafa ya kila aina yanayosababishwa na hali ya hewa yameshuhudiwa miaka ya hivi karibuni kwa namna ambayo litakuwa kosa kubwa kutowajibika ipasavyo hivi sasa.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Gakuba, Daniel