Mabalozi wa Ulaya waahidi kuwasaidia wakimbizi Nyarugusu
2 Juni 2021Mabalozi hao ni pamoja na Balozi wa Ujerumani Bi Regine Hess, Balozi wa Uholanzi Bw. Jeroen Verheul, Balozi wa Denmark Bw. Mette Nirgaard, Balozi wa Uswiss Bw. Didier Chassot, Balozi Ubelgiji Bw. Peter van Acker na Balozi wa Uingereza David Concer.
Katika ziara hiyo wakimbizi wamelalamikia viongozi hao kwa kutoa misaada isiyokidhi mahitaji hususani chakula na kuni za kupikia pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bi. Regine Hess ametumia fursa hiyo kuutaarifu umma wa wakimbizi kuwa Ujerumani itaendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo udhamini wa elimu ya juu, afya na chakula kupitia mashirika yanayohudumia wakimbizi ya UNHCR, WFP, IRC na Save the Children.
Waiomba EU kuongeza misaada
Pamoja na kuzishukuru serikali ya Tanzania, UN na Umoja wa Ulaya, wakimbizi wa Burundi na DRC wameungana na mweyekiti wa kambi ya Nyarugusu Bi. Abilola Angelique kuomba Umoja wa Ulaya utafakari kuongeza misaada hasa ya chakula ambacho kimepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 32 na hivyo kusababisha adha na njaa kwa familia.
Soma pia: Ujerumani yasaidia utunzaji mbuga za wanyama Tanzania
Changamoto nyingine zilizotajwa na wakimbizi hao hasa vijana ni ukosefu wa ufadhili wa elimu, zana za michezo, kufutwa kwa siku ya vijana kwa wakimbizi na uhuru mdogo wa kutoka nje ya kambi kwa ajili ya kutafuta mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula.
Pamoja na maeneoo mengine mabalozi hao wametembelea kituo cha watoto kinachosimamiwa na shirika la Save the Childreni kwa ufadhili wa serikali ya Ujerumani kupitia shirika la maendeleo la Ujerumani GIZ ambapo watoto hufundishwa michezo mbalimbali pamoja na stadi za maisha.
Balozi Regine Hess ameridhishwa na maendeleo ya kituo hicho na kuahidi kuwa serikali ya Ujerumani itaendelea kutoa misaada ya kiutu ili kunusuru maisha ya watoto hao na wakimbizi kwa Ujumla
Nchi za Umoja wa Ulaya ndio wafadhili wakubwa wa misaada ya mahitaji mbalimbali kwa wakimbizi wa Burundi na DRC nchini Tanzania.
Mwandishi: Prosper Kwigize