Ujerumani yasaidia utunzaji mbuga za wanyama Tanzania
10 Mei 2021Hii ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili yenye historia ndefu.
Fedha hizo ambazo ni zaidi ya bilioni hamsini za kitanzania zinalengwa kutumika katika kulinda ikolojia pamoja na kuimarisha mahusiano na majirani wanaoishi karibu na hifadhi hizo ambazo ziliwahi kupata tuzo kadhaa za kimataifa kutokana na kuwa na wanyama wa kuvutia wakubwa kama vile Simba, Tembo, na hata Twiga ambao wanaongeza kuvutia watalii.
Fedha zitatumika kulinda ikolojia katika hifadhi
Akizungumza wakati akikagua miradi mbalimbali balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess amesema, janga la virusi vya Corona limeitikisa dunia na sekta ya utalii kwa kiwango kikubwa imeathirika hivyo hakuna budi kuhakikisha jitihada zinafanyaka ili kuendeleza utalii.
Balozi Hess amesema fedha hizo zitatumika katika kulinda ikolojia katika hifadhi hizo, ambazo zimekuwepo kwa kipindi kirefu sasa. aliongeza
Mradi huo unaokwenda kwa jina la ufadhili wa dharura katika kulinda na kuhifadhi bioanuwai nchini Tanzania, utatekelezwa na taasisi za serikali ambazo zina dhamana ya moja kwa moja na wanyama pori ikiwemo mamlaka ya uhifadhi nchini TANAPA pamoja na mamlaka ya usimamizi wanyama pori tanzania TAWA.
Miradi itakwenda kwa kipindi cha miaka mitatu
Aidha serikali ya Tanzania imesema miradi ambayo itatekelezwa na fedha hizo ni ya kipindi cha miaka mitatu na mbali na kulinda ikolojia ya hifadhi hizo zitalenga kuimarisha mahusiano baina ya vijiji jirani na mbuga hatua ambayo itapunguza kiwango cha uvunaji haramu wa wanyama hao pori.
Waziri wa utalii Damas Ndumbalo amesema miradi iliotolewa fedha hizo itakwenda kwa kipindi cha miaka mitatu na kisha watafanya tathmini ya pamoja kuangalia mafanikio yaliofikiwa.
Itakumbukwa Ujerumani imekuwa mshirika mkubwa wa tanzania na kwa muda mrefu katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori, ambapo katika kipindi cha miaka mitano hivi karibuni zaidi ya euro milioni 106 sawa na zaidi ya shilingi za tanzania bilioni 300 zimetolewa katika kuunga mkono juhudi hizo.