LONDON: Wito wa kuchukua hatua zaidi kulinda mazingira
5 Novemba 2006Zaidi ya watu 20,000 waliandamana siku ya Jumamosi mjini London wakitaka juhudi zaidi za kisiasa kuhusu mazingira.Maandamano hayo yametangulia mkutano wa kimataifa utakaofunguliwa siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa Kenya Nairobi,juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Waandamanaji wametoa mwito kwa Uingereza,iongoze kwa njia ya mfano na ipendekeze sheria mpya ili kila mwaka kiwango cha gesi ya kaboni dayoksaidi izidi kupunguzwa nchini humo.Maandamano hayo vile vile yalipita mbele ya ubalozi wa Marekani, kulalamika dhidi ya uamuzi wa rais George W.Bush wa kutotia saini Mkataba wa Kyoto unaotoa mwito wa kupunguza gesi zinazoongeza ujoto na kuathiri hali ya hewa.Ripoti iliyotolewa na Uingereza juma hili,imeonya juu ya hatari ya kutokea janga la kiuchumi duniani,pindi hatua za kutosha hazitochukuliwa,kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.