Ifahamu UNRWA na majukumu yake Ukanda wa Gaza
30 Januari 2024Kufuatia tuhuma hizo za Israel, mataifa kadhaa yanayolifadhili shirika hilo la Umoja wa Mataifa, zikiwemo Ujerumani, Marekani, Uingereza na Australia yalitangaza kusitisha misaada yao, licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuyatolea wito kuhakikisha yanaendelea kuwasaidia wakimbizi wa Palestina, ambao tangu hapo walishakuwa kwenye hali mbaya.
Mkuu wa shirika hilo, Phillippe Lazzarini, anasema watu milioni mbili kwenye Ukanda wa Gaza wanategemea msaada wa moja kwa moja kutoka shirika hilo, na kwamba uwezo wake wa kuwahudumia sasa unaporomoka.
Lakini shirika hilo maalum kwa wakimbizi wa Kipalestina, ambalo kifupisho chake ni UNRWA, ni nini?
UNRWA ilibuniwa mwaka 1949, mwaka mmoja tu baada ya kuundwa kwa dola la Israel na baada ya kuanza kwa vita vya Mashariki ya Kati kati ya taifa hilo jipya na mataifa ya Kiarabu. Lilianza kazi rasmi mwezi Mei 1950.
Lengo la kuanzishwa kwake ni kutoa msaada kwa zaidi ya Wapalestina 700,000 ambao walifukuzwa kutoka ardhi zao wakati wa kuundwa kwa Israel na kufuatia vita hivyo vya mwaka 1948.
UNRWA inasadia kuhakikisha wakimbizi wapatao milioni sita wa Kipalestina waliochawanyika nchini Jordan, Syria, Lebanon, Ukingo wa Magharibi na Ukindo wa Gaza wanapata elimu, huduma za afya na ustawi wao.
Kwa mujibu wa mkuu wa shirika hilo, Lazzarini, kwa wakimbizi hao, UNRWA ndio pumzi yao.
Nusu ya bajeti ya shirika hilo inaelekezwa kwenye elimu, ambapo UNRWA inaendesha zaidi ya skuli 700, likiwa shirika pekee la Umoja wa Mataifa ambalo lina mfumo kamili wa masomo.
Vipi UNRWA inapata ufadhili wake?
Shirika hilo linafadhiliwa kwa kiasi kikubwa na michango ya hiyari kutoka kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa. Mnamo mwaka 2022, ahadi iliyotolewa kwa UNRWA ni dola bilioni 1.17, nusu yake ikitoka kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mwezi Januari 2023, shirika hilo liliomba nyongeza ya bajeti ya dola bilioni 1.6, lakini kufikia mwezi Mei lilikuwa limepokea ahadi ya dola milioni 364 tu, yaani asilimia 25 pekee ya kile linachokihitajia.
Kwa takribani muongo mzima sasa, UNRWA imekuwa inaendeshwa kwa nakisi ya bejeti tangu kuundwa kwake.
Soma pia:Nchi kadhaa zasitisha ufadhili kwa UNRWA
Iliuanza mwaka 2023 ikiwa na deni la dola milioni 75. Miongoni mwa sababu ni ongezeko la idadi ya wakimbizi wa Kipalestina, kwani vizazi vya wakimbizi hao nao pia wana haki ya hadhi ya ukimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Mwaka 2018, Marekani - ambayo ilikuwa mchangiaji mkubwa - ilikata ufadhili wake kwa amri ya aliyekuwa rais wa wakati huo, Donald Trump, ambaye alikuwa akiukosowa Umoja wa Mataifa na shirika hilo kwa ujumla. Washington ilirejesha misaada yake baadaye.
Hadi ilipositisha ufadhili wake kutokana na tuhuma za Israel, Marekani ilikuwa ndiyo mchangiaji mkubwa zaidi, ikifuatiwa na Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Sweden.
Utata wa UNRWA uko wapi?
Trump na wanasiasa wa siasa kali za mrego wa kulia wa Israel, akiwamo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, wanaikosoa fasili ya nani anaweza kuchukuliwa kuwa mkimbizi wa Kipalestina inayofahamika na shirika hilo.
UNRWAinasema wakimbizi wa Kipalestina ni "watu ambao nyumbani kwao kulikuwa ni Palestina baina ya tarehe 1 Juni 1946 hadi 11 Mei 1948, na ambao walipoteza makaazi yao na njia za kujikimu kutokana na mzozo wa 1948.
" Tovuti ya UNRWA pia inaeleza kwamba "Vizazi vya wakimbizi wa kiume wa Kipalestina, wakiwemo watoto wa kulea, wana haki pia ya kusajiliwa."
Netanyahu anasema UNRWA ni shirika la kudumisha wakimbizi, akitaka livunjwe, kwa madai kuwa kazi hii haipaswi kufanywa na Umoja wa Mataifa.
Soma pia:UN kuwaadhibu watakaobainika kuhusika na "ugaidi"
UNRWA inasema hata ikifugwa, wale wanaotambuliwa kuwa wakimbizi wataendelea kuwa wakimbizi wa Kipalestina kwa mujibu wa Azimio 194 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.