Hali ya kiutu kusini mwa Gaza yakaribia kuwa 'mbaya zaidi'
5 Desemba 2023Hali bado ni tete katika ukanda wa Gaza ambako jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi yake. Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa DW eneo hilo, hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi'.
Wakati Israel ikitanua operesheni zake eneo la kusini mwa Ukanda huo, jeshi la nchi hiyo limewaambia wakaazi, ambao wengi wao walikuwa tayari wamekimbia ghasia kaskazini mwa Gaza , wawe wanaangalia mtandaoni ili kufahamu ni maeneo gani yatakayolengwa kila siku na mashambulizi.
Mwandishi wa DW mjini Jerusalem Rebecca Ritters ameeleza kuwa watu wa Gaza wamepewa aina fulani ya ramani ambayo imegawanywa kwa miraba. Kila eneo lina namba na wameambiwa waangalie sehemu walipo kwenye ramani hiyo kutokana na namba hizo na kila siku watapewa orodha ya maeneo ambayo yatalengwa kwa mashambulizi na hivyo watu watatakiwa kuhama.
Mwandishi huyo ameongeza kuwa tatizo ni kwamba watu wa Gaza hawana sehemu ya kwenda na wanakosa mahali pa kukimbilia na kujificha. Watu wengi pia huenda wasiweze kupata mawasiliano ya intaneti ili kupokea ujumbe huo na kufahamu ni mahala gani patakuwa salama siku hiyo.
Wito wa Shirika la Msalaba Mwekundu na taarifa za UN
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Mirjana Spoljaric, ambaye aliwasili Gaza jana Jumatatu amesema mateso ya watu wa Gaza 'hayavumiliki' huku akitoa wito wa raia kulindwa kwa mujibu wa sheria za vita na kuruhusu misaada kuingia Gaza bila vikwazo.
Wito kama huo umetolewa pia na Berlin. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani Sebastian Fischer amesema wanatarajia Israel itatoa ulinzi "halisi" kwa raia wa Gaza na kwamba sio tu kuwataka raia kuondoka kwenye eneo la hatari, lakini kuhakikisha wako katika nafasi nzuri ya kupata makazi salama mahali pengine.
Soma pia: Israel yatanua vita Gaza Kusini hofu ikitawala kuhusu vifo vya raia
Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa umesema asilimia 80 ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema karibu watu milioni 1.9 ikiwa ni sawa na asilimia 80 ya wakazi wote huko Gaza wameyakimbia makazi yao tangu Oktoba 7.
Vituo vya UNRWA havikuepuka mashambulizi huko Gaza. Jumla ya vituo vya kazi 30 vimelengwa moja kwa moja huku 55 vikishuhudia uharibifu. Hata hivyo shirika hilo halikueleza ni nani aliyehusika na mashambulizi katika mitambo yao. Pia, takriban wafanyakazi 111 wa UNRWA wameuawa huko Gaza tangu vita vilipozuka kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Hamas tarehe 7 Oktoba.
Vita vikiendelea, Israel imewataka raia wake kuchukua tahadhari wanaposafiri katika mataifa 80 duniani ikiwa ni pamoja na yale ya Magharibi mwa Ulaya kama Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.
Baraza la Usalama la Taifa la nchi hiyo (NSC) limechukua uamuzi wa kuzidisha viwango vya tahadhari na limetoa rai kwa raia wake kuepuka safari zisizo za lazima katika mataifa kama Eritrea, Afrika Kusini, nchi kadhaa za kiarabu na zile za Mashariki ya Kati hasa zinazopakana na Iran, kusini mwa Urusi, na nchi kadhaa za Kiislamu barani Asia.
NSC imesema tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, kumekuwa na ongezeko katika juhudi zinazofanywa na Iran na washirika wake ili kuyalenga maslahi ya Israel na kuwadhuru Wayahudi kote duniani.