1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korti kuu yasema EU inaweza kuzinyima pesa Hungary na Poland

16 Februari 2022

Mahakama ya juu ya Umoja wa Ulaya, imeamua kuwa jumuiya hiyo inaweza kusimamisha malipo ya msaada kwa nchi wanachama ikiwa zitakiuka kanuni za utawala wa sheria,huku ikitupilia mbali pingamizi la Hungary na Poland.

https://p.dw.com/p/477j9
Luxemburg | EuGH Gebäude
Picha: Alexandre Marchi/MAXPPP/dpa/picture alliance

Serikali za mrengo wa kulia za mataifa hayo zilihoji kwamba hatua kama hiyo haikuwa na msingi wa kisheria. Mataifa hayo mawili, wapokeaji wakubwa wa Fedha za Umoja wa Ulaya, yamkuwa yakizidi kukosolewa katika miaka michache iliyopita, kwa kupuuza kanuni za magharibi za kuheshimu maadili ya kidemokrasia katika mataifa yao.

Hukumu hiyo ilikuwa inatarajiwa pakubwa na wengi walioyashtumu mataifa hayo mawili kwa kuzorotesha demokrasia na waliiona hatua hiyo kama silaha muhimu zaidi kwa Umoja wa Ulaya kuzuwia kuongezeka kwa mpasuko wa uhalali wa kidemokrasia ndani ya kanda hiyo.

Linapokuja suala la kanuni za kidemokrasia," Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa na uwezo wa kuyalinda maadili hayo ndani ya mipaka ya mamlaka yake," ilisema mahakama katika hukumu yake.

Europäische Kommission AstraZeneca Gerichtsverhandlung
Chumba kikuu cha mahakama ya sheria ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: Virginia Mayo/AP/picture-alliance

Soma pia: Umoja wa Ulaya utasimama kidete dhidi ya ukaidi wa Poland

Halamashauri kuu ya Umoja wa Ulaya  ilisema ingesubiri hukumu ya Jumatano kabla ya kufanya maamuzi juu ya kuzuwia ufadhili, lakini rais wa halmashauri kuu hiyo Ursula von der Leyen aliikaribisha mara moja hukumu hiyo.

"Halmashauri Kuu italinda bajeti ya Umoja wa Ulaya dhidi ya ukiukaji wa kanuni za utawala wa sheria. Tutafanya kazi kwa dhamira," aliahidi von der Leyen.

Hata Hivyo Hungary ilijibu hukumu hiyo kwa haraka, ambapo waziri wake  wa sheria Judit Varga ameshutumu uamuzi huo kwenye ukurasa wake wa Facebook, na kuuita ``hukumu ya kisiasa'' na kwamba ni uthibitisho kwamba Umoja wa Ulaya unatumia  vibaya mamlaka yake.

Varga  amesema hukumu hiyo ni matumizi mengine ya shinikizo dhidi yao kama nchi kwa sababu "tulipitisha sheria yetu ya ulinzi wa watoto wakati wa majira ya joto," akimaanisha sheria yenye utata ya Hungary iliyopitishwa mwaka jana, ambayo inakataza uonyeshaji wa ushoga au mabadiliko ya kijinsia kwa watoto katika maudhui za vyombo vya habari.

Soma pia:EU kuzishinikiza Poland na Hungary kuhusu hatma ya bajeti 

Hungary na Poland huko nyuma zilisema kwamba mahakama inavuka mamlaka yake katika kuidhinisha utaratibu mpya ambao haukueleza katika mikataba ya Umoja wa Ulaya. Zilisema kuweka kiunganishi kama hicho kati ya ufadhili na maamuzi ya kisheria ya nchi wanachama ilikuwa sawa na vitisho kutoka Brussels.

Poland na Hungary zinakabiliwa na ukosoaji Umoja wa Ulaya kwa miaka mingi, kuhusiana na madai ya kuingilia uhuru mahakama na vyombo vya habari, miongoni mwa kanuni nyingine za demokrasia.

Umoja wa Ulaya umejikuta ukishindwa kufanya mengi ili kubadili muelekeo wa lolote kati ya mataifa hayo, na hivyo kufanya kuheshimu maadili ya kidemokrasia kama sharti la kupewa fedha.

Frankreich EU Polen Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.Picha: Ronald Wittek, Pool Photo/AP/picture alliance

Soma pia: Maelfu waandamana Poland kupinga sheria tata

Kuheshimu utawala wa kidemokrasia na sheria ndio msingi wa kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, na mahaka ilisisitiza kuwa, baada ya kuingia katika umoja huo, kanuni hizo lazima zizingatiwe.

"Mahakama inaainisha, kwanza, kwamba usimamiaji wa maadili hayo hauwezi kupunguzwa na kuwa wajibu tu ambao taifa linalotaka kuwa mwanachama linapaswa kutimiza ili kuingia Umoja wa Ulaya, na ambao linaweza kupuuza baada ya kuingia," ilisema mahakama.

Huko Hungary, Waziri Mkuu Viktor Orban amekuwa akishinikiza kile alichokiita “Demokrasia isiyo ya kiliberali,'' ambayo wakosoaji wake wanasema ni sawa na kuminya demokrasia.

Nchini Poland, chama cha Sheria na Haki kinaidhibiti pakubwa serikali na pia kinazidi kukabiliwa na ukosoaji kutoka kwa mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Serikali ya mrengo wa kulia nchini humo imevunja sheria za taifa hilo ili kupata nguvu ya  kisiasa kwa kudhibiti mahakama na majaji.

Awali Hungary na Poland zilitaka kuzuia bajeti kwa sababu ya kuanzishwa kwa utaratibu mpya, lakini mwishowe zilikubaliana na mpango huo kwa sharti kwamba Mahakama ya Haki ya Ulaya itaupitia upya.

Chanzo: AP