Kongamano la tisa la miji ya Bara Afrika lafanyika Kisumu
17 Mei 2022Akizungumza kwenye kongamano la miji ya Bara Afrika la Afri Cities mjini Kisumu,Kenya mjumbe mteule wa maswala ya miundo mbinu na maendeleo katika muungano wa Bara Afrika AU Raila Odinga anasema, Benki ya Afrika inakadiriwa kuwa, Bara la Afrika lina kiasi cha shilingi bilioni 170 kwa mwaka na hivyo kusisitiza kuwa, pana haja ya Bara hili kubuni mfuko wa pamoja wa fedha za maendeleo.
Ameongeza, kuwa, licha ya hili, mapungufu ya fedha pia ni takriban dola 110 ambazo zinaweza kufunikwa kwa ushirikiano mataifa ya Bara Afrika. "Afrika inaweza kujitosheleza katika kujifadhili ili isiwe inategemea ufadhili kutoka taasisi za kifedha za kimataifa au makubaliano ya kiserikali ambayo wakati mwingine ni ya gharama ya juu kwa mataifa ya Afrika,” alisema Raila Odinga.
Mwenyekiti muungano wa Bara Afrika AU, Moussa Faki Mahamat naye amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Bara Afrika kushirikiana kwa kuangazia miradi ya pamoja kama vile ya barabara, bandari, anga miongoni mwa zingine.
Pia anasema, ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kuangazia ongezeko la watu wanaohamia mijini na kujipanga na hivyo mkutano wa Afri Cities unastahili kuwa mwamko mpya.
Mkurugenzi Mtendaji - mpango wa Makaazi katika Umoja wa Mataifa UNHABITAT – Maimuna Mahmoud Shariff amehimiza umuhimu wa kuimarisha miji midogo Barani Afrika ili kukabiliana na ongezeko la watu ikizingatiwa kuwa, kufikia mwaka 2050 asilimia 50 ya iadi ya watu wanaoishi maeneo ya mashinani watahamia sehemu za mijini.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyefungua rasmi kongamano hilo amehimiza umuhimu wa Bara Afrika kuungana ili kutafuta suluhu dhidi ya changamoto zinazokabili bara hili. Kongamano la Afri cities linaingia siku yake ya pili hiyo kesho na linatazamiwa kukamilika tarehe 21 jumamosi wiki hii.
Mwandishi: Musa Navie DW Kisumu