1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Dunia kuanza leo nchini Brazil

Admin.WagnerD12 Juni 2014

Baada ya matatizo ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa viwanja, na kutumia bajeti ya kupindukia katika maandalizi, hatimaye hii leo mashindano ya kombe la dunia la soka yanaanza kutifua vumbi nchini Brazil.

https://p.dw.com/p/1CHAS
Kocha wa Brazil Scolari na nyota wa timu ya nchi hiyo, Neymar katika mkutano na waandishi wa habari mjini Sao Paolo
Kocha wa Brazil Scolari na nyota wa timu ya nchi hiyo, Neymar katika mkutano na waandishi wa habari mjini Sao PaoloPicha: Reuters

Brazil inaamini kwamba hali ya mvutano wa kijamii iliyofuatia matatizo katika maandalizi ya kombe la dunia itamalizika mara tu timu yao itakapoanza kupata ushindi, huku wakitarajia kuwa tafrija zitaanza leo iwapo wataweza kuikandika Croatia katika mechi ya ufunguzi.

Wabrazil wengi walikasirishwa na ripoti kwamba serikali yao ilitumia kiasi cha dola bilioni 11.3 katika kuandaa mashindano hayo, huku huduma za kijamii zikipewa bajeti isiyotosha. Rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff amekanusha madai hayo, na kuongeza kwamba anao uhakika Brazil itafanya vyema ndani ya uwanja, na nje yake pia wakati wa mashindano haya.

Hata baadhi ya mashabiki, akiwemo Rogerio Souza aliyezungumza na shirika la habari la Reuters, wanaamini kwamba furaha itagubika nafasi ya manung'uniko ikiwa timu yao itafanya vyema, huku wakionya kuwa ikishindwa kutamba, malalamiko yataongezeka.

Jinamizi la maandamano

Maafisa nchini Brazil wanao wasiwasi kwamba maandamano na msongamano wa magari, vinaweza kuwatatiza baadhi ya mashabiki ambao watakwenda kwenye sherehe za ufunguzi ambazo zitaanza saa 17 jioni nchini Brazil, sawa na saa tatu usiku maeneo ya Afrika Mashariki.

Brazili imekumbwa na maandamano ya kupinga gharama ya maandalizi ya kombe la dunia
Brazili imekumbwa na maandamano ya kupinga gharama ya maandalizi ya kombe la duniaPicha: Reuters

Serikali imeitangaza leo kuwa siku ya mapumziko katika juhudi za kuyapunguza matatizo hayo, lakini ukweli kwamba itakuwepo misafara ya wageni mashuhuri wakiwemo wakuu wa nchi 10 na maafisa waandamizi wa shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA, una maana kwamba usumbufu barabarani hautaepukika.

Kutokana na tofauti ya muda kati ya Brazil na sehemu nyingine za dunia ikiwemo Afrika, mashabiki wengi watakumbwa na kadhia ya kuzitazama mechi saa za usiku, baadhi zikichezwa usiku wa manane. Hata hivyo kwa mujibu wa mchambuzi wa soka nchini Tanzania Maulid Kitenge ambaye amezungumza na DW, muda sio tatizo kwa mashabiki.

Nchi tano zabeba matumaini ya Afrika

Bara la Afrika linawakilishwa na timu tano katika mashindano haya, ambazo ni Cameroun, Ghana, Nigeria, Cote d'Ivoire na Algeria. Cameroun ndio itakayokuwa ya kwanza kutoka Afrika kushuka uwanjani, ikijipima misuli na Mexico kesho Ijumaa saa moja usiku saa za Afrika Mashariki.

Timu ya Ghana ni miongoni mwa zile zinazobeba matumaini ya waafrika
Timu ya Ghana ni miongoni mwa zile zinazobeba matumaini ya waafrikaPicha: Getty Images

Timu ya Ujerumani ambayo ni miongoni mwa timu bora katika mashindano haya, itacheza mechi yake ya kwanza Jumatatu ijayo, dhidi ya Ureno inayoongozwa na nahodha wake Christiano Ronaldo. Itakuwa saa moja usiku Afrika Mashariki.

Kwa mechi ya ufunguzi jioni ya leo, mengi yanatarajiwa kwenda kama ilivyopangwa. Hata hali ya hewa inatabiriwa kuwa ya kupendeza, bila mvua wala joto kali.

Brazil ambayo mashabiki wengi wa soka wanaichukulia kama makao makuu ya kiroho ya kabumbu, itamtegemea sana mshambuliaji wake mwenye umri wa miaka 22, Neymar, na mechi ya leo dhidi ya Croatia itakuwa kipimo kwa uwezo wa timu hiyo yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya kombe la dunia, na ambayo wengi wanatabiri kuwa inayo nafasi kubwa ya kulitwaa kombe la mwaka huu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu