Maandamano yavuruga msisimko wa soka
10 Juni 2014Tamasha la fainali za kombe la dunia linaloanza Alhamis tarehe 12 limekabiliwa na maandamano ya umma wa Brazil ukidai hali bora zaidi ya maisha. Katika mwaka 2007, ukweli kwamba Brazil ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya shirikisho la kimataifa la kandanda FIFA mwaka huu 2014 kulizusha shangwe kubwa kitaifa. Lakini hali hiyo inaonekana kufifia kutokana na migomo na maandamano yanayoongezeka kabla ya tamasha hilo.
Ilionekana kuwa ni makubaliano mazuri wakati ule, lakini mambo yalibadilika. Maelezo ya ununuzi wa kinu cha kusafisha mafuta cha Marekani mwaka 2006, moja kati ya kashfa za sekta ya mafuta inayoikabili serikali ya Brazil, inaweza pia kuingia katika fainali hizi za FIFA za kombe la dunia. Tukio hilo kubwa la michezo linaweza kuwa kilele cha kiuchumi cha taifa hili linaloinukia kwa nguvu za kiuchumi, ambalo lilishinda mara nyingi kombe la dunia, mara tano katika majaribio mara 18.
Lakini hivi sasa , badala ya kupanga sherehe za kuzikaribisha nchi zinazoshiriki katika tamasha hilo linaloanza Juni 12 hadi Julai 13, Wabrazil wanaingia mitaani katika maandamano ambayo yanazuwia barabara na kusababisha miji kushindwa kufanya shughuli zake, wakifanya migomo kudai ongezeko la mishahara, na wakilalamika kuhusu rushwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika wakati wa kazi za ujenzi wa kutayarisha tukio hilo kubwa duniani.
Nchi hiyo ya kandanda na furaha inaipa mgomo starehe hiyo inayopendwa nchini humo.
Mjini Rio de Janeiro , mitaa michache iliyopambwa kwa rangi za kijani na njano, rangi za timu ya taifa, zinaonekana kuwa kinyume na sherehe hizo pamoja na hisia za matarajio kabla ya fainali zilizopita za kombe la dunia. Hamasa imekuwa chini wakati huu Brazil inakuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa duniani.
Sononeko la Wabrazil lilizuka Juni 2013, kwa mshangao na mara nyingi maandamano ya ghasia dhidi ya utendaji mbovu katika mfumo wa afya na elimu, usafiri wenye mvurugiko, rushwa, na fedha nyingi zikitumika kwa matayarisho ya fainali za kombe la dunia.
Wakihofu kuongezeka zaidi kwa ghasia , serikali imeamuru kuwekwa kwa polisi 157,000 pamoja na vikosi vya jeshi kuhakikisha usalama wakati wa michezo hiyo ambayo itafanyika katika miji 12 katika nchi hiyo kubwa yenye wakaazi karibu milioni 200.
Kupungua kwa shauku kuhusu soka ni hali ambayo imeonekana katika fainali tatu za kombe la dunia, amesema Paulo Santos , ambaye ni kinyozi kwa muda wa miaka 40 sasa katika eneo la watu wa tabaka la chini mjini Rio de Janeiro na anasikia mawazo ya wateja wake mia kadha, katika kile kinachoonekana kama ukusanyaji wa maoni usio rasmi.
Kuwa mwenyeji wa kombe la dunia kungepaswa kuamsha shauku ya wapenzi wa soka.
Lakini wanafanya tamasha hili kwa fedha za watu wengine sio zetu, amelalamika Santos, akiakisi hisia zilizozagaa kwamba zoezi lote hilo limekuwa likifuatiwa na kashfa za rushwa, ubadhirifu wa fedha za umma na uroho wa FIFA.
Uchunguzi unaakisi mtazamo huu. Mwezi Februari , asilimia 52 tu ya wale waliohojiwa na taasisi ya kukusanya maoni ya Datafolda ,iliyounga mkono kuwa Brazil kuwa mwenyaeji wa fainali za kombe la dunia, ikiwa ni chini kutoka asilimia 79 mwaka 2008. Uchunguzi wa hivi karibuni , ambao ulifanyika katika mji wa kusini wa Sao Paulo tu, uligundua kuwa asilimia 45 ya walioulizwa wanapendelea na asilimia 43 wanapinga, wakati waliobaki wamesema hawajali.
Mwandishi: Sekione Kitojo / IPS
Mhariri: Josephat Charo