Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam akanusha kutaka kujiuzulu
3 Septemba 2019Kwa mujibu wa sauti zilizovuja, Lam anasikika akiwaeleza viongozi wa wafanyabiashara aliokutana na wiki iliyopita kwamba amesababisha "uharibifu usiosameheka", pale alipowasilisha muswada wa kuwashitaki wahalifu China bara.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku ya Jumanne, uliorushwa moja kwa moja kupitia televisheni, Lam amesema hajawahi kufikiria kuiomba China kujiuzulu kwasababu serikali ya Beijing ina imani na serikali yake katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro uliodumu kwa miezi mitatu bila ya kuingilia.
"Sijawahi kuwasilisha barua ya kujizulu kwa serikali ya watu wa China. Sijafikiria hata kufanya mazungumzo ya kujiuzulu na serikali ya China. Chaguo la kutojiuzulu ni la kwangu", alisema Lam.
Lam ameongeza kuwa ameshangazwa na kauli aliyoitoa katika mkutano wa faragha wa wiki iliyopita kuvuja. Katika sauti hizo kiongozi huyo wa Hong Kong anasikika akisema uwezo wake wa kuutafutia ufumbuzi mgogoro "umefikia ukingoni" kwa sababu sasa anawatumika mabwana wawili akiongeza kuwa suala hilo tayari limefika katika ngazi ya kitaifa.
Lakini katika mkutano wake na waandishi wa habari, Lam anasema serikali yake ina imani na serikali ya China katika kuumaliza mgogoro huo. "Lakini nilijiambia mara kwa mara katika kipindi cha miezi mitatu kwamba mini na timu yangu lazima tubaki ili kuisaidia Hong Kong. Kuisaidia Hong Kong katika hali ngumu, na kuwatumikia watu wa Hong Kong. Huo unabaki kuwa msimamo wangu".
Maandamano zaidi
Wanafunzi wa shule na vyuo mjini Hong Kong, wanaingia siku ya pili ya mgomo wa masomona kuendelea na maandamano. Hatua hii inakuja baada ya vurugu kubwa kabisa kutokea mwishoni mwa juma tangu ghasia zilipoongezeka zaidi ya miezi mitatu iliyopita. Waandamanaji walichoma vizuizi vya barabarani na kurusha mabomu ya petroli na polisi wakiwajibu kwa maji ya kuwasha na kuwapiga virungu. Waandamanaji wanataka uhuru zaidi kwa koloni hilo la zamani la Uingereza ambalo lilirejeshwa kwa China mwaka 1997 chini mfumo wa nchi moja, mifumo miwili. Mifumo hiyo inawapatia uhuru mpana ikiwemo haki ya kuandamana na mahakama huru.
Hata hivyo, wana hofu kwamba uhuru huo hivi sasa unaanza kuingiliwa taratibu na chama cha kikomunisti cha China, madai ambayo China inayakana. Polisi imewakamata karibu watu 900 tangu maandamano yalipoanza, wakiwemo wanaharakati maarufu.
reuters/AP