Wanafunzi Hong Kong wasusia masomo, kuendelea na maandamano
2 Septemba 2019Mgomo huo unafuatia wikiendi iliyotawaliwa na vurugu tangu ghasia hizo zilipoongezeka miezi mitatu iliyopita. Katika vurugu za mwishoni mwa juma, waandamanaji walichoma vizuizi na kurusha mabomu ya petroli na polisi walijibu kwa kuwarushia gesi ya kutoa machozi na kuwapiga virungu. Maandamano mapya yamepangwa mchana wa leo(Jumatatu) kwa wanafunzi kukwepa masomo na kumiminika katika bustani za umma.
Kikosi cha kutuliza ghasia kilikuwa kikipiga doria siku ya Jumatatu katika maeneo ya treni za chini ya Ardhi, ambako vurugu za hivi karibuni zilianzia. Mamia ya wanafunzi walikusanyika nje ya chuo kikuu cha Chinese University of Hong Kong, mojawapo ya vyuo vikubwa, wakitoa hotuba ya kuhamasisha na kuonyesha mshikamano kwa ajili ya maandamano ya kudai demokrasia. Waziri wa elimu Kevin Yeung ametoa onyo kwa wanafunzi hao.
"Shule hazipaswi kutumiwa kama sehemu ya madai ya kisiasa au kujaribu kuishinikiza serikali katika masuala ya kisiasa. Tungependa kuendelea kuzifanya shule kuwa tulivu na mahali salama kwa ajili ya wanafunzi kusoma", alisema Kevin.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha mistari ya vijana wakijipanga nje ya shule huku wakibeba mabango. Hata hivyo shule nyingi za msingi zilikuwa zimefungwa kutokana na tahadhari ya kimbunga. Jumatatu ya leo ilikuwa ni ya kwanza baada ya msimu wa likizo ya majira ya joto kumalizika.
Waandamanaji waliitisha mgomo mkubwa lakini watu wengi wameonekana kurejea katika shughuli zao za kila siku huku maduka yakifunguliwa, safari za treni kuendelea na wafanyakazi kuingia ofisini. Hata hivyo siku ya Jumapili, maelfu ya waandamanaji walizuia barabara na usafiri wa umma wa kwenda uwanja wa ndege wa Hong Kong, katika jaribio la kumulikwa zaidi kimataifa ili kuishinikiza China kutoa uhuru zaidi kwa koloni hilo la zamani la Uingereza.
Mamlaka ya uwanja wa ndege ilisema safari 25 zilisisitishwa siku ya Jumapili lakini usafiri umerejea katika hali ya kawaida. Baada ya kuondoka uwanja wa ndege siku ya Jumapili baadhi ya waandamanaji, walivamia vituo vya treni za chini ya ardhi na kuharibu kamera za kiusalama, CCTV pamoja na taa.
Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lamambaye amekuwa kiini cha hasira ya waandamanaji kwa serikali ya jiji wanayodai inadhibitiwa na China, aliandika kupitia Facebook kwamba vituo 10 vya treni viliharibiwa na waandamanaji. Polisi na waandamanaji walikabiliana usiku wa Jumamosi katika baadhi ya maeneo.
AP/Reuters