Kimbunga Haiyan magazetini
11 Novemba 2013Kimbunga Haiyan, mkutano wa usafi wa mazingira nchini Poland na mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizohodhi magazeti ya Ujerumani.
Tuanze na janga lililosababishwa na kimbunga kikubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa kilichoangamiza maisha na mali katika visiwa vya Ufilipino.Kimbunga hicho kilichopewa jina Haiyan ingawa kimepungua kasi kidogo,hakijasita,kinaelekea Vietnam.Misaada ya dharura inahitajika linaandika gazeti la "Badische Neueste Nachrichten":"Misaada ya haraka ya dharura haitosaidia kudhamini ,mafuriko mengine,dharuba nyengine au zilzala nyengine zisitokee na kusababisha maisha zaidi ya binaadam kuangamia na maafa zaidi kuenea.Ili kupunguza madhara makubwa yanayosababishwa na majanga,jumuia ya kimataifa itabidi ikubaliane. Wakaazi wa dunia wanaozidi kuongezeka wanahitaji kinga dhidi ya majanga yasiyokadirika ya kimaumbile.Hata kama kinga hiyo haitatosha kikamilifu hata hivyo isiwe dhaifu kwa namna ambayo daima mafukara tu ndio wanaodhurika zaidi."
Kumbukumbu za Mchamungu Martin
"Kuanzia leo bata mzinga wa kuchoma ndio chakula kikubwa majumbani.Na leo pia watoto wakibeba mwenge,wanaimba majiani wakijiwekea matumaini ya kuzawadiwa peremende na biskuti.Kawaida hilo ni tukio la maana kabisa.Leo ni siku ya kumkumbuka mchamungu Martin;hata katika visiwa vya Ufilipino.Zaidi ya robo tatu ya wakaazi wa visiwa hivyo ni wakatoliki.Ndio maana na wao pia wanamjua mchamungu Martin aliyevua koti lake la baridi,msimu wa baridi na kumfunika mtu asiyejimudu.Hii leo wafilipino milioni nne na laki tatu wanajikuta wamepoteza kila walichokuwa nacho.Wako katika shida kwasababu kimbunga kimewaangamizia msingi wa maisha yao.Makoti ya baridi pekee hayatoshi-panahitajika mapeni hata kama si vizuri kusema hivyo."
Nchini Poland unaanza hii leo mkutano wa kimataifa kuhusu usafi wa mazingira.Gazeti la "Thüringischen Landeszeitung" linaandika:
Walimwengu wazindukane
Hata kama hofu za maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi zimezidi kuongezeka,hata hivyo hali ya kuregeza kamba imeanza kujitokeza tangu ulipofanyika mkutano kama huo mwaka 2011 mjini Durban nchini Afrika kusini .Na nchini Ujerumani pia.Katika kampeni za uchaguzi mkuu,suala la kuzidi hali ya ujoto katika sayari yetu halikupewa umuhimu wowote.Hata katika mijadala kupitia televisheni wagombea kiti cha kansdela hawakulidhukuru suala hilo.Kwakuwa Ujerumani haiungi mkono mipango ya Umoja wa Ulaya ya kuanzishwa sheria inayolazimisha kiwango cha chini cha moshi unaotoka ndani ya magari,haiwezi kwa hivyo nchi hii kuangaliwa kama mshika bendera wa wanaopigania usafi wa mazingira.
Nani atakabdhiwa wadhifa gani?
Mada ya mwisho magazetini inahusu majadiliano ya kuunda serikali kuu ya muungano kati ya vyama ndugu vya Christian Democratic Union-CDU,Christian Social Union CSU na wana Social Democratic wa SPD.Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika:"Haina maana yeyote kujipasua kichwa tangu sasa kutaka kujua chama gani kitakabadhiwa wizara gani na nani atashika wadhifa gani.Hata hivyo eti eti hazishi.Kwanini?Labda kwasababu majina na sura ni rahisi kuzungumzia badala ya mada tofauti na tete zinazojadiliwa hivi sasa.Kimoja watu wanabidi watambue:kuunda serikali kunahitaji subira."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef