1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ataka uwekezaji zadi Misri

Mohammed Khelef13 Machi 2015

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amesifu mageuzi ya uchumi chini ya utawala wa Rais Abdel Fatah al-Sisi wa Misri akiwatolea wito wawekezaji kuwekeza licha ya changamoto za kiusalama.

https://p.dw.com/p/1EqOn
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.Picha: Mark Wilson/Getty Images

Akilihutubia Baraza la Biashara la Marekani kandoni mwa kongamano la uwekezaji unaofanyika kwenye mji wa ufukweni wa Sharm El-Sheikh, Kerry amesema uwekezaji zaidi wa kigeni unaweza kuisaidia Misri kuinua kwa kasi kiwango chake cha ukuwaji wa uchumi.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani alisema Misri imekuwa ikifanya mageuzi ya kimsingi kwa mwaka mzima sasa, ikiwemo kukata ruzuku ya mafuta na kupitia upya mfumo wa kodi.

Kerry ameahidi msaada wa Marekani kwa ajili ya mageuzi makubwa zaidi ya kiuchumi, ambao amesema utaisaidia kufanya biashara iwe rahisi zaidi nchini Misri sambamba na kulinda uwekezaji wa kigeni.

"Marekani ina hamu sana, iko tayari na ina nia ya kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi ya Misri na tunaziheshimu juhudi ambazo tayari mmechukua na tunataka kuwasaidia," alisema Kerry.

Mengi yanahitajika kufanyika

Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kifedha Duniani (IFC), Jin-Yong Cai, amesema ingawa hatua za maendeleo zinaonekana nchini Misri, bado nchi hiyo ina mengi zaidi ya kufanya kufikia lengo, ikiwemo uimarishaji wa sera na kanuni zinazoongoza uwekezaji.

Misri inatazamia kuwa kongamano hili litashajiisha uwekezaji kwenye uchumi wake ambao bado unaendelea kujijenga upya baada ya miaka takribani mitano ya mkwamo wa kisiasa kufuatia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011, yaliyomuondosha madarakani Rais Hosni Mubarak.

Rais Abel Fattah al-Sissi wa Misri.
Rais Abel Fattah al-Sissi wa Misri.Picha: imago/Xinhua

Waziri wa Uwekezaji, Ashraf Salman, aliliambia shirika la habari la Reuters nchi yake inatazamia kuwa kongamano hilo litaiwezesha Misri kupata makubaliano ya kibiashara yenye thamani ya hadi dola bilioni 20.

Mkutano na Sissi, Mfalme Abdullah, Rais Abbas

Pamoja na kuhudhuria kongamano hilo, Kerry atakutana pia Mfalme Abdullah wa Jordan, Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas na Rais Sissi wa Misri.

Katika mkutano wake na Rais Sissi, Kerry atazungumzia pia masuala ya usalama katika mkoa wa Sinai na nchi jirani ya Libya na kupata nguvu kwa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

Hata hivyo, hatazamiwi kutoa ahadi yoyote ya msaada wa kijeshi katika ziara hiyo ya siku mbili, licha ya Rais Sissi kutoa wito wa kupatiwa msaada huo kukabiliana na Dola la Kiislamu.

Marekani ilikuwa ikiipa Misri msaada wa kijeshi wa dola bilioni moja na nusu kila mwaka, na bado ni miongoni mwa mataifa matatu ambayo ni washirika wakubwa wa kibiashara wa Misri, huku viwanda vya Marekani vikiwa chanzo cha pili cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Daniel Gakuba