Uhusiano wa Qatar na Misri wazidi kuingia dosari
19 Februari 2015Afisa mmoja katika wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar amesema wamemuita nyumbani balozi wa nchi hiyo kufuatia taarifa iliotolewa na mjumbe wa Misri katika Jumuiya ya kiarabu, Tariq Adel, aliyeishutumu Qatar kwa kuunga mkono Ugaidi, baada ya muakilishi wa Qatar kusita kutoa maoni juu ya tamko lililokaribisha hatua ya Misri kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Libya.
Aidha Mkurugenzi wa masuala ya kiarabu katika wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar Saad bin Ali al-Mohannadi amesema nchi yake haikutaka kutoa maoni ya haraka juu ya mashambulizi yaliofanywa na Misri akisisitiza ilifaa paweko na mashauriano kabla ya hatua ya kijeshi kuchukuliwa dhidi ya taifa jirani.
Mohannadi ameongeza kuwa hatua iliochukuliwa huenda ikawaathiri raia wasiokuwa na hatia. Hata hivyo amesema Qatar inaunga mkono na itaendelea kuunga mkono matakwa na utulivu wa watu wa Misri.
Qatar mpaka sasa inapinga kuondolewa madarakani rais wa zamani wa Misri Mohammed Mursi na bado inaendelea kutoa hifadhi kwa wanachama wa chama cha udugu wa kiislamu cha kiongozi huyo wa zamani.
Uhusianao kati ya Qatar na Misri umezorota katika miaka ya hivi karibuni kufuatia Qatar kumuunga mkono Mohammed Mursi.
Mapema Jumanne ndege za kivita za Misri aina ya F-16 zilishambulia maeneo yanayoshikiliwa na wanamgambo mjini Derna Libya baada ya kundi hilo la wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu kutoa mkanda wa Video ulioonyesha mauaji ya waumini wa madhehebu ya Koptic raia wa Misri wakiuwawa kwa kukatwa vichwa. Waumini hao walikuwa wamesafiri katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika kutafuta ajira.
Libya yataka iondolewa vikwazo vya silaha ili ipambane na wanamgambo wa IS
Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Libya amelitaka baraza la Usalama la Umoja wa Mataiafa kuiondolea vikwazo vya silaha nchio hiyo ili iweze kupambana na wanamgambo wa dola la kiislamu, wakati linapojaribu kukita mizizi Kaskazini mwa Afrika na kujaribu kusogea mbele kuingia ulaya.
Hata hivyo kamati ya Umoja ya mataifa inayoshughulikia maombi kama hayo ya Libya ya kutaka kuondolewa vikwazo vya silaha vilivyowekwa mwaka wa 2011, inasita kuchukua hatua hiyo kufuatia wasiwasi kwamba huenda silaha hizo zikaangukia mikononi mwa wanamgambo.
Libya imekumbwa na mapigano makali tangu kuondolewa na kuuwawa kwa kiongozi wake Moammar Gaddafi mwaka wa 2011.
Kwa sasa kuna serikali mbili na mabunge mawili yanayohasimiana ambapo kila moja linadhibitiwa na wanamgambo tofauti.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP
Mhairiri Mohammed Abdul-Rahman