Kenya yatoa siku 14 kuzifunga kambi za wakimbizi
24 Machi 2021Hatua ya serikali ya Kenya kutoa muda huo wa wiki mbili kwa shirika la UNHCR kufunga kambi hizo za wakimbizi,imetafsiriwa kama iliyochochewa na mgogoro baina yake na Somalia.
Serikali ya Kenya na ya Somalia, zimekuwa katika mgogoro wa kidiplomasia baada ya Somalia kuishitumu Kenya kwa kuingilia maswala yake ya ndani. Hili kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kiusalama George Musamali,huenda ndiyo chanzo cha Kenya kutaka kuidhibu Somalia.
soma zaidi: Kenya kufunga Dadaab baada ya miezi sita
Musamali ameiambia DW kwa njia ya simu kwamba,hatua ya Kenya inakwenda kinyume na mkataba wa kimataiafa kuhusu wakimbizi ambayo inalinda haki zao.
Aidha,anahoji kwamba,muda wa wiki mbili uliotolewa na serikali wa kufungwa kwa kambi hizo hautoshi kuwahamisha wakimbizi kutoka kwenye kambi zenyewe
"Haya malumbano ambayo tumeshuhudia baina ya serikali ya Nairobi na Mogadishu ndiyo suala ambalo limechangia hatua inayochukuliwa hivi sasa na serikali ya Kenya.Hatua hiyo ni kinyume na mkataba wa Geneva na nadhani mashirika ya kimataifa yataingilia kati na jinsi ilivyofanyika hapo awali,hili swala halitaona mwangaza wa mchana,” alisema George Musamali
Hakuna nafasi ya mazungumzo kuhusu kufungwa kwa kambi hizo
Waziri wa usalama wa taifa Dakta Fred Matiang'i jana jumanne aliwasilisha uamuzi wa serikali ya Kenya kwa mwakilishi wa umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi hapa nchini Fathiaa Abdalla.
Waziri huyo aliripotiwa kuujulisha ujumbe wa UNHCR kwamba,hakuna nafasi ya mazungumzo kuhusu kufungwa kwa kambi hizo.
soma zaidi: Wakimbizi kambi ya Dadaab Kenya wapo mashakani.
Bi Fathiaa Abdalla aliomba muda wa kushauriana na wakuu wake japo akaahidi kuwa,UNHCR iko tayari kupunguza idadi ya wakimbizi kwenye ardhi ya Kenya.
Hatua ya kenya kutaka kuzifunga kambi za wakimbizi haijapokelewa vyema na wakimbizi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma katika jimbo la Turkana. Mwaka 2013, serikali ya Kenya ilikuwa imekubaliana na Somalia kuwarejesha wakimbizi nchini mwao katika kipindi cha muda wa miaka mitatu.
Siku ya ijumaa, wizara ya mambo ya kigeni ya Kenya itafanya mashauriano na mabalozi kutoka mataifa mengine ambayo raia wake wamo kwenye kambi hizo za wakimbizi. Hili ni jaribio la pili kwa serikali ya Kenya kutaka kuzifunga kambi za wakimbizi ili wakimbizi wote warejeshwe makwao.
Mwandishi: Michael Kwena/DW Kakuma