Katibu mkuu wa UN, aonya juu ya mabadiliko ya tabia nchi
1 Desemba 2019Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Jumapili kwamba juhudi za ulimwengu kuzuia mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kikubwa hazitoshi kufikia sasa na kuna hatari ya hali ya joto duniani huenda ikapindukia kiwango ambacho hakiwezi kudhibitiwa.
Kauli ya katibu mkuu Guterres ameitowa kabla ya kufunguliwa Jumatatu mkutano wa wiki mbili wa kimakuhusu mazingira utakaofanyika mjini Madrid Uhispania.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema athari za kupanda kwa viwango vya joto ikiwemo hali mbaya ya hewa tayari imeanza kushuhudiwa kote duniani ambapo athari za kutisha zinawaandama binadamu na viumbe hai vingine.
Amegusia kuhusu ulimwengu kuwa na ufahamu wa kisayansi na njia za kiteknolojia za kukabiliana na kudhibiti viwango vya joto duniani lakini kinachokosekana ni nia ya kisiasa. Akizungumza mjini Madrid Guterres amesema hali ya kutodhibitiwa tena kwa viwango vya joto haiko mbali na inatunyemelea.
Wajumbe kutoka takriban nchi 200 watajaribu kupitia na kukamilisha sheria zinazousimamia mkataba wa Paris uliofikiwa mwaka 2015 katika mkutano huo unaoanza tarehe 2 mpaka 13.
Na miongoni mwa yatakayoshughulikiwa ni pamoja na kuangalia jinsi ya kuanzisha mifumo ya kibiashara ya kimataifa inayofanya kazi ya kudhibiti viwango vya utoaji gesi zinazochafua mazingira pamoja na kuzilipa fidia nchi masikini kwa hasara ilizoingiakutokana na kupanda kwa viwango vya kina cha maji ya baharini pamoja na athari nyinginezo za mabadiliko ya tabia nchi.
Ama mkuu wa Umoja wa Mataifa amegusia juu ya ushahidi wa kisayansi unaoonesha athari zinazotokana na gesi chafu inayotengenezwa na binadamu abazo tayari zinaonekana duniani ikiwa ni pamoja na joto kali na kuyeyuka kwa barafu katika eneo zima la kusini mwa bara la Antarctic.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Tatu Karema