1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani kulihutubia taifa kuhusu Corona

18 Machi 2020

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema Kansela Angela Merkel atalihutubia taifa katika hotuba itakayopeperushwa mubashara Jumatano kuelezea hali halisi ilivyo nchini humo juu ya mripuko wa virusi vya Corona

https://p.dw.com/p/3ZeiE
Deutschland Berlin | Coronavirus | Pressekonferenz Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Kiongozi huyo wa Ujerumani anatarajiwa kutoa hamasa kwa raia wake kuendelea kufuata maagizo yaliotolewa na serikali kubakia nyumbani, baada ya taifa hilo kubwa kiuchumi barani Ulaya kutangaza mikakati mipya ya kuweza kupunguza virusi hivyo kusambaa nchini Ujerumani.

Kando na hotuba yake anayoitoa kila wakati wa mkesha wa mwaka mpya, hii itakuwa ni mara ya kwanza ndani ya miaka yake 15 aliyohudumu kama Kansela kuwahutubia raia moja kwa moja kupitia televisheni ya ARD na ZDF.

Msemaji  huyo wa serikali Steffen Seibert amesema Kansela Merkel hatozungumzia mikakati mengine ya kukabiliana na virusi vya Corona ila atakugusia kile kinachopaswa kufanyika wakati huu nchini Ujerumani kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo na kile kila mmoja anachopaswa kufanya kufanikisha hilo.

Serikali kuu yachukua hatua ya kufunga mikusanyiko ya hadhara

Berlin | Angela Merkel und Frank-Walter Steinmeier
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Siku ya Jumatatu serikali kuu pamoja na serikali za majimbo zilitangaza mikakati iliyoathiri maisha ya umma, kwa kufunga maduka na mikusanyiko ya kidini.

Maduka ya vitu muhimu kama vyakula, madawa na mabenki ni miongoni mwa maduka yatakayobakia wazi huku mabaa, vilabu, maeneo ya kuogelea, na majumba ya sinema yakitakiwa kufungwa kama tahadhari ya kuzuwia maambukizi ya virusi vya Corona.

Kansela huyo wa Ujerumani Angela Mwerkel na Rais Frank-Walter Steinmeier wameendelea kuwahimiza raia wa Ujerumani kubakia nyumbani na kufuta likizo zao ndani na nje ya nchi. Ujerumani ni miongoni mwa Mataifa yalioathirika vibaya kwa janga la virusi vya Corona huku takwimu za hivi karibuni zikionyesha vifo vya watu 12 na maambukizi kufikia zaidi ya 8000 kutoka watu 1000.

Rais wa taasisi ya Robert Koch (RKI) Lothar Wieler ametahadharisha iwapo Ujerumani haitoweza kuzuwiya maingiliano ya watu katika wiki kadhaa zijazo, inawezekana ujerumani ikawa na visa hadi milioni 10 vya watu wanaougua virusi hivyo ndani ya miezi mitatu ijayo.

Chanzo: afpe