Kampuni 6 za kichina matatani DRC
6 Septemba 2021Wakati wa kikao kilichofanyika hii leo mjini Bukavu, idara ya mashauriano ya asasi za kiraia imelaani kile unachokiita unyonyaji haramu wa madini na uvamizi wa mashamba ya wakaazi na kampuni hizo za kigeni katika wilaya ya Mwenga, muungano huu wa raia ukiendelea kusikitikia hali ya kwamba haki za binadamu zinakiukwa na sheria ikikanyagwa chini ya macho dhaifu ya mamlaka.
Asasi za kiraia hapa Kivu Kusini zinazidi kujiuliza maswali ni nani anayefaidika na uchimbaji haramu wa dhahabu na madini mengine unaofanywa na Wachina ambao kama inavyoonekana hawajali kuizingatia hatua ya gavana wa mkoa wa Kivu Kusini inayowataka kusimamisha shughuli zao kwa muda.
Kinachozusha maswali zaidi ni barua ya waziri husika na madini nchini Kongo aliyomwandikia gavana wa Kivu Kusini Théo Ngwabidja hivi karibuni, akimtaka kusitisha harakati ya kuzisimamisha kampuni hizo za Kichina, akisema kwamba gavana huyo hana mamlaka kufanya hivyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari leo mjini Bukavu, kiongozi wa ofisi ya uratibu wa mashirika ya kiraia katika mkoa wa Kivu Kusini, Adrien Zawadi amewataka viongozi wa Kongo kuwajibika zaidi, kufanya uchunguzi kwa kina na kutoa mwangaza kuhusu sakata hili.
UDPS yataka uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika waadhibiwe
Upande wa chama tawala cha UDPS cha Rais Félix Tshisekedi, wanachama wanataka pia uchunguzi ufanyike kwa kina, na wahusika waadhibiwe kulingana na sheria za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Waziri mpya wa madini katika mkoa wa Kivu Kusini, Appolinaire amesema kuwa suala la uchimbaji wa madini unaofanywa na kampuni za Kichina linafuatiliwa, akiahidi pia kwamba gavana Ngwabidje atahakikisha sheria inayohusu uchimbaji wa madini nchini Kongo inafuatwa.
Wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri Ijumaa, Waziri Mkuu wa Kongo Jean-Michel Sama Lukonde aliitaka serikali kuwachukulia hatua wahusika wa hali hii ambayo kama alivyosema, inarahisisha pia uwepo wa vikundi vyenye silaha ambavyo vinazuia udhibiti wa serikali katika eneo la Mwenga.
Balozi wa China mjini Kinshasa, Zhu Jing amelaani pia uchimbaji haramu wa madini ya Kongo akiihakikishia serikali ya Kongo kwamba China iko tayari kushirikiana na mamlaka ya Kongo kukomesha tabia hiyo.
Mwandishi: Mitima Delachance, DW, Bukavu.