Juhudi za kupunguza uchafuzi wa mazingira
14 Novemba 2006Hayo ni maoni ya wajumbe wanaohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Nairobi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Katika mkutano huo mjini Nairobi,fikra mbali mbali zimesikika;kama vile teknolojia na misaada itolewe kwa nchi masikini zitakazopunguza gesi zinazochafua mazingira,malengo maalum yawepo kwa viwanda kama vile vya vyuma au aluminiamu na mikopo itolewe ili kuzuia uharibifu wa misitu katika mabonde ya Amazon na Kongo.Kwa maoni ya mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusika na mabadiliko ya hali ya hewa,Yvo de Boer,”Ni muhimu kuzivutia nchi hizo ili baada ya mwaka 2012,nchi hizo zipate kuungana na Mkataba wa Kyoto ambao huweka vipimo vya gesi zinazotolewa na viwanda na kuchafua mazingira.
Mkataba wa Kyoto huzishurutisha nchi 35 zinazoendelea,kuwa hadi ifikapo miaka ya 2008 na 2012,zipunguze gesi zinazochafua mazingira kwa asili mia 5 kulinganishwa na kile kipimo cha mwaka 1990.Nchi nyingi zilizotia saini mkataba wa Kyoto zingependa kuona gesi hizo zikipungzwa zaidi, lakini vile vile madola zaidi yaungane na Mkataba wa Kyoto.De Boer anasema baadhi ya fikra za kuvutia madola zaidi,huenda zikasaidia kuzima upinzani wa rais George W.Bush wa Marekani alieitoa nchi yake kwenye makubaliano ya Kyoto hapo waka 2001.Lakini mjumbe wa Marekani,Harlan Watson amesema,Marekani haina mpango wa kutia saini Mkataba wa Kyoto hivi sasa au baada ya mwaka 2012.Hayo,licha ya kwamba,Marekani ni mzalishaji mkubwa kabisa wa gesi zinazochafua mazingira,ikiwa mbele ya Uchina.Uchafuzi huo hasa unasababishwa na mitambo ya nishati,viwanda na magari.Mkataba wa Kyoto ni hatua ya mwanzo ya kuzuia kile ambacho wanasayansi wengi wanasema litakuwa vurugu kubwa kabisa katika hali ya hewa kama vile mafuriko,kuongezeka kwa ujoto pamoja na hali ya ujangwa na vile vile vimo vya bahari vitaongezeka.
Baadhi ya nchi zinazoendelea,kuanzia Papua New Guinea hadi Bolivia,zinataka msaada kama tuzo ikiwa zitapunguza mwendo wa uharibifu wa misitu.Kwa mfano,mratibu wa “Ofisi ya Maendeleo ya Usafi wa Taifa” kutoka Bolivia,Gisela Ulloa amesema nchi yake inafanya iwezavyo kuhifadhi misitu na hatua hiyo inasaidia hali ya hewa kwani miti inapokuwa hutumia kaboni-dayoksaidi inayokusanya ujoto.
Wakati huo huo Umoja wa Ulaya unasema hadi mwaka 2020,wanachama wake lazima wapunguze uzalishaji wa gesi zinazochafua hewa,kwa asilimia 15 hadi 30 kulinganishwa na kile kipimo cha mwaka 1990.