1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Nigeria lashambulia shabaha za Boko Haram

17 Mei 2013

Vikosi vya serikali vimeanza kuzishambulia ngome za wapiganaji wa Kiislamu kaskazini-mashariki mwa Nigeria, katika operesheni ya kurudisha maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa kundi la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/18Zn4
Wanajeshi wa Nigeria wakifanya mazoezi kabla ya kuanza operesheni dhidi ya Boko Haram.
Wanajeshi wa Nigeria wakifanya mazoezi kabla ya kuanza operesheni dhidi ya Boko Haram.Picha: picture-alliance/dpa

Duru kutoka jeshi la Nigeria zimesema kuwa wanajeshi walivamia maeneo yaliyoko katika hifadhi ya wanyama ya Sambisa, eneo la vijijini lenye ukubwa wa kilomita za mraba 500 katika jimbo la Borno, ambako wapiganaji wa Kiislamu wamepiga kambi. Katika maandalizi zaidi ya mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyoko katika majimbo matatu ambako rais Goodluck Jonathan alitangaza hali ya hatari siku ya Jumanne, jeshi la Nigeria pia lilipeleka ndege za kivita na helikopta za kijeshi katika kanda hiyo.

Baadhi ya uharibifu unaosababishwa na mashambulizi ya Boko Haram mjini Maiduguri.
Baadhi ya uharibifu unaosababishwa na mashambulizi ya Boko Haram mjini Maiduguri.Picha: picture-alliance/dpa

Makundi ya haki za binaadamu yaliezea hofu juu ya usalama wa raia kutoka pande mbili, lakini hatua ya rais Jonathan inaungwa mkono na umma, baada ya zaidi ya miaka mitatu ya kujaribu kutuliza uasi huo bila mafanikio ya kueleweka. Operesheni dhidi ya waasi hao inafuatia kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali na waumini wa dini ya kikristu kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, yanayofanywa na wapiganaji hao wa Kiislamu, ambao wanataka kuanzisha utawala unaofuata sheria za Kiislamu nchini Nigeria.

Ndege na helikopta kusaidiana na vikosi vya ardhini

Raia milioni 170 wa Nigeria, ambayo ndiyo nchi yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika, wamegawanyika sawa sawa kati ya Waislamu ambao ndiyo wengi zaidi kaskazini, na Wakristu walio wengi zaidi kusini. Kulikuwepo na taarifa kidogo kutoka hifadhi ya Sambisa, ambayo imeshawahi kushambuliwa hapo kabla na vikosi vya serikali kwa lengo la kuwafurusha waasi mwezi Februari.

Hali ya hatari iliyotangazwa na rais Jonathan inaathiri majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa, ambayo yanapakana na nchi za Niger, Chad na Cameron yenye ukubwa wa kilomita za mraba 150,000, eneo sawa na Uingereza au jimbo la Illinois nchini Marekani, lakini lenye wakaazi milioni 10 tu.

Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakari Shekau.
Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakari Shekau.Picha: AP

Msemaji wa jeshi la anga la Nigeria, Yusuf Anas alithibitisha kuwa ndege na helikopta za kivita zimetumwa katika eneo hilo kusaidiana na vikosi vya ardhini, huku chanzo kutoka jeshi la nchi hiyo kikisema huenda kukawa na mashambulizi ya angani dhidi ya vituo vya Boko Haram.

Huduma za simu katika majimbo ya Borno na Yobe zilikatwa kabisaa siku ya Alhamisi. Katika jimbo la Adamawa ambako amri ya kutotembea usiku ilitangazwa, baadhi walikaribisha operesheni hiyo kwa tahadhari. Uasi wa kundi la Boko Haram umesha gharimu maisha ya maelfu ya watu tangu uanze mwaka 2009, wakati ukandamizaji ulipoua watu 800, akiwemo mwanzilishi wa kundi hilo Mohammed Yusuf, aliefariki akiwa katikakizuizi cha polisi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,ape
Mhariri: Saum Yusuf Ramadhan