1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Je,Trump ataondolewa kuwania urais mnamo Januari 6?

14 Septemba 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anakabiliwa hivi sasa na mkururo wa kesi ikiwemo kadhaa za jinai, hilo linatazamwa na wachambuzi wa siasa kama kisiki kwa mwasiasa huyo asietabirika katika hotuba zake.

https://p.dw.com/p/4WL0J
Rais wa zamani wa marekani Donald Trump
Rais wa zamani wa marekani Donald TrumpPicha: Joed Viera/AFP/Getty Images

Lakini mwanasiasa huyo ndiye anaongoza kura za maoni ya umma za wanaowania kupeperesha bendera ya chama cha Republican kwenye uchaguzi wa rais mwaka ujao.

Tayari kuna nadharia zinazotajwa kwamba zinaweza kutumika kumzuia mwanasiasa huyo machachari kuingia tena ikulu ya White House. 

Hakuna mwanasiasa aliyekalia kuti kavu hivi sasa nchini Marekani kumshinda Donald Trump.

Rais huyo wa zamani wa taifa hilo anaandamwa kila kona na kesi mahakamani, tangu masuala binafsi kama kumnyamazisha mwanamke mmoja mcheza filamu za ngono asitibue kampeni yake ya mwaka 2016 hadi zinazohusu jaribio lake la kupindua matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2020.

Soma pia:Harris: Trump hataachwa kuwajibishwa ghasia za Capitol Hill

Kuna kesi nyingine kubwa inayonukia kuhusu dhima ya kiongozi huyo katika tukio la kuwamiwa majengo ya bunge la Marekani mnamo Januari 6 mwaka 2021.

Tukio hilo linatajwa kuwa lilifanywa na wafuasi wa Trump kutokana na shinikizo lake. 

Wapinzani wa Trump wanachochea kesi hizo?

Wapinzani wa Trump wanajenga hoja kuwa shambulizi dhidi ya majengo ya Bunge linatosha kumchorea mstari mwekundu mwanasiasa huyo kutokanyaga ikulu ya White House kama rais wa Marekani. 

Hoja zao zimejikita kwenyemabadiliko ya 14 ya katiba ya Marekani inayolifanya tukio hilo la kushambuliwa taasisi ya kidemokrasia kuwa sawa na uasi dhidi ya dola. 

Baadhi ya waataalum wa sheria wanasema matendo ya Januari 6 yanamwondolea moja kwa moja Trump sifa za kuwania urais.

USA Wahlen 2024 Donald Trump
Rais wa zamani wa marekani Donald Trump akiwa katika mikutano yake ya kisiasaPicha: Sue Ogrocki/AP Photo/picture alliance

Wanadurusu hotuba kali ya Trump aliyoitoa mbele ya wafuasi wake ambao baadae waliyavamia majengo ya bungekujaribu kuzuia mchakato wa Joe Biden kuidhinishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2020.

Wanasema ibara ya 3 ya makabadiliko ya 14 ya katiba ya Marekani inazuia maafisa wa serikali waliohusika na "uasi au kuanzisha vurumai ya kuiangusha serikali" kamwe kutochukua wadhifa wa urais. 

Soma pia:Timu ya kampeni ya Trump yachangisha dola milioni 7.1 baada ya picha yake kusambazwa

Kundi moja la kiraia la Citizens for Responsibility and Ethics la mjini Washington tayari lilifungua kesi huko Colarado mapema mwezi huu  kutaka maafisa wanaosimamia uchaguzi wa jimbo hilo kutomweka Trump kwenye karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa Novemba mwaka ujao. 

Mashauri kama hayo dhidi ya maafisa wanaosimamia uchaguzi kwenye majimbo ya Marekani yanaweza kufuata kwa kutumia kipengele hicho tata cha katiba ambacho bado haijawahi kutumika kumzuia mtu kushika wadhifa wa uongozi wa serikali ya shirikisho.

Hata hivyo yafaa kukumbusha kuwa hadi sasa Trump bado hajafunguliwa mashtaka wala kutiwa hatiani kwa uasi au vurumai ya Januari 6.

Anakabiliwa na kesi nne za jinai zinazohusiana na jaribio lake la kupindua matokeo ya uchaguzi uliopita lakini zote hazihusiani na tukio la kuvamiwa majengo ya bunge.

Wanasheria: Kumzuia Trump kugombea kutazusha wasiwasi

Wataalamu wengine wa  sheria wanasema juhudi zozote za mkuzuia Trump kuwania uchaguzi ujao zitatengeneza tabia ya kutia wasiwasi.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

Kwamba viongozi wanaosimamia uchaguzi kwenye majimbo watakuwa na nguvu zisizoulizwa na yeyote za kuwazuia wagombea tena kwa tafsiri yao wenyewe kuhusu suala la "uasi au dhamira ya kuingusha serikali"

Kuwaondoa wagombea kwenye mchakato wa uchaguzi kwa makosa ambayo hawajatiwa hatiani au hata kushatikiwa nayo, kunaweza kutafsiri kuwa mchezo mchafu dhidi ya haki zao na ulinzi sawa ambao kimsingi unalindwa na mabadiliko ya 14 ya katiba ya Marekani.

Soma pia:Trump ashikiliwa na kupigwa picha ya rekodi za polisi

Hata iwapo hilo litatokea bado kuna mjadala ni vipi linataanza kufanya kazi.

Baadhi ya wanazuoni wa sheria wanasema itahitaji sheria iliyotungwa na bunge kuwezesha wagombea kuondolewa kwenye kinyangányiro kwa misingi ya kupoteza sifa kwa kushiriki kwao uasi.

Lakini wataalamu wengine wanasemaitakuwa ni hati ya mahakama ndiyo itawapa nguvu maafisa wanaosimamia uchaguzi kuamua nani atakuwemo kwenye sanduku la kura.  

Lakini hilo la bila kuwepo sheria litakuwa ni mchakato mrefu.

Makundi ya kiraia itafaa wawashawishi wasimamizi wa uchaguzi kwenye majimbo 50 ya Marekani kutoweka jina la Trump kwenye karatasi la kura au kufanya hivyo kwa majaji ili watoe amri ya kuzuia jina la Trump lisiwemo kwenye uchaguzi ujao.

Uwezekano wa hilo kufanikiwa ni suala la kusubiri na kuona.